TFF KWAWAKA MOTO, CAG kukagua Rasilimali watu na Fedha

MATANGAZO

MATANGAZO
SERIKALI imeagiza Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali ‘CAG’ kufanya ukaguzi wa Rasilimali watu na fedha katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kupunguza minong’ono ya wizi wa fedha.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi za shirikisho hilo jana, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Waziri.

“Sheria inamruhusu Msajili wa Vyama vya Michezo na Baraza la Michezo (BMT) kukagua mali na hesabu hivyo nimewaagiza mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ili aje kufanya ukaguzi wa mali za TFFm ikiwemo rasilimali watu na hesabu zote,” alisema Nape.
Pia Nape alisema ukaguzi ukishafanyika utaondoa dhana potofu ambayo imejijenga kwa baadhi ya watu kuwa fedha zinazotoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na zile zinazotokana na wafadhili zinatumika vibaya.
Nape alimweleza Rais wa TFF, Jamal Malinzi kuwa anapata ujumbe mfupi kuwa wafanyakazi hawajalipwa mishahara kwa miezi mitatu, jambo ambalo Malinzi alikiri na kutolea ufafanuzi.
“Wafanyakazi wanadai mshahara wa mwezi mmoja kwani Julai wamelipwa ila kocha mkuu wa timu ya Taifa Stars, Charles Mkwasa na msaidizi wake Hemed Moroco wanatudai lakini hadi Oktoba tutakuwa tumewalipa,” alisema Malinzi.
Katika hatua nyingine, Waziri Nape alizungumzia mchakato wa mabadiliko kwenye klabu kongwe za Simba na Yanga na kusema kuwa serikali inabariki lakini akatahadharisha taratibu na sheria zifuatwe.
“TFF usisubiri mpaka jipu liive ukiwa umekunja mikono ukiangalia mambo yakienda ovyo ni lazima mhakikishe uuzwaji unakuwa wazi, sheria na taratibu zinafuatwa ili kuondoa harufu ya rushwa na haki za wanachama waliokuwa wamiliki kabla zilindwe,” alisema Nape.
“Mtu anamiliki mkono halafu anatangaza anauza mkono halafu anaununua tena mwenyewe, haiwezekani lazima ajiondoe kwenye ushindani ili haki na sheria zifuatwe,” alisema.
Nape alisema serikali inafuatilia kwa makini mchakato mzima hatua kwa hatua ili haitasita kuingilia pale ambapo sheria zinakiukwa.
Aidha Waziri Nape alisema watashirikiana na TFF kutatua mgogoro wa Stand United ili kunusuru ustawi wa maendeleo ya soka na kuahidi kuzungumza na mdhamini wa timu hiyo ACACIA waendelee kuidhamini.
Pia ameagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa makini na chaguzi za mikoa na uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo utakaofanyika mwakani ili kuziba mianya yote ya rushwa ili kuwapata viongozi bora.