Aliyekuwa Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wenzake 8 Wafikishwa Mahakamani
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na maofisa wengine saba waandamizi, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka 27 yakiwamo ya matumizi mabaya ya ofisi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 1.2.
Washitakiwa wengine ni Mkurugenzi wa Huduma za Kibiashara, Avelin Momburi, Meneja wa Fedha na Uhasibu, Benamini Mwakatumbula, Meneja wa Bajeti na Milki, Joseph Makani, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima na Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.
Wengine ni Xavery Kayombo ambaye wadhifa wake haukutajwa, na Astery Ndefe ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers Company Limited. Washitakiwa hao pia wanakabiliwa na mashitaka yanayohusu kutumia nyaraka zenye kusudio la kudanganya na kula njama za kutenda kosa.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote dhidi ya mashitaka hayo kwa sababu wanashitakiwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi. Wote waliamuriwa kurejeshwa mahabusu hadi Agosti 31, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
Uchunguzi wa kesi hiyo kwa mujibu wa waendesha mashitaka, wanaoongozwa na Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Awamu Mbangwa haujakamilika.
Hakimu alisema kwamba suala la dhamana litaamuriwa na Mahakama Kuu, kwa kuwa kiwango cha fedha katika kesi hiyo kinazidi Sh milioni 10.
Lakini alisema atatoa uamuzi kuhusu dhamana kwa washitakiwa Mobuli na Makani kesho kwa sababu ya hoja kwamba wawili hao hawakabiliwi na mashitaka ya uhujumu uchumi, kama washitakiwa wengine.
Jopo la waendesha mashitaka linawajumuisha pia Leonard Swai, Janeth Machuria, Joseph Kiula na Fatma Waziri.
Waendesha mashitaka walidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2010 na 2015, wakiwa watumishi wa umma, Maimu na Mwakatumbula walitumia vibaya madaraka yao kwa kuidhinisha kwa Kampuni ya Gotham International Limited malipo ya Dola za Marekani milioni 5.175 pamoja na Sh milioni sita.
No comments:
Post a Comment