Barua kwa Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye
Habari mheshimiwa waziri, nina imani ni mzima wa afya, pole na hongera kwa kazi ngumu unayofanya kwa moyo mmoja katika wizara yako. Mimi ni kati ya wananchi tuliojiajiri katika tasnia ya filamu hapa nchini, japo hali ni mbaya mno lakini tunaendelea kujikongoja hivyo hivyo tukisubiri uharamia ukomeshwe kwa asilimia kubwa ili tupumue kidogo kama watu wa shuguli zingine za kiuchumi.
Mheshimiwa kisa cha kushika hii kalamu ni baada ya kusoma habari za kukamatwa kwa vijana wa Orijino Komedi hapo majuzi kwa kosa la kuvaa sare za jeshi la polisi kitendo ambacho ni kinyume na sheria za nchi yetu. Lengo ni kuzungumzia hilo suala ila kwakuwa hii nafasi ya kuongea na wewe ni adimu, acha nitaongeza na mengine kidogo nje ya suala la sare.
Mheshimiwa mlivyosema kurasimisha tasnia ya filamu nina imani mlimaanisha kwa ujumla wake, lakini kuna kipindi nashawishika kuwa maana ya kurasimisha iliishia kwenye kuweka stika za TRA kwenye kava za DVD basi. Maana mi ninaamini kama tasnia ingerasimishwa katika ujumla wake na ikafuatiliwa haswa, mpaka muda huu tungekuwa pazuri maana muda umepita kidogo mheshimiwa
Kwa suala la sare mheshimiwa ni kitu kidogo mno ambacho kama kweli kuna urasimishaji, kusingekuwa na tatizo kama la Orijino Komedi sasa hivi. Najua kuna wazo linaweza kuja kuwa wale mabwana wamevaa kwenye harusi kwahiyo wana makosa na hoja yangu kuwa sio ya msingi hapa. Orijino Komedi wanajulikana kazi yao na pale walikuwepo kazini bila kujali walilipwa au walimfanyia free mwenzao. Ile ni kazi ya sanaa, ila cha muhimu wamefanya kitu ambacho wamezua mjadala na labda tuombe Mungu ndio uwe mwanzo wa kujadili kati ya wadau wa filamu na serikali kuhusu mambo hayo ambayo ndio mjumuiko sahihi wa maana ya urasimishaji.
Nilisema sare ni jambo rahisi kwa sababu tunataka hadi silaha zenyewe, sio sare tu. katika filamu kuna kutumia bunduki zenyewe au za bandia zinazofanana na za halisi(pellets guns), mheshimiwa tunahitaji vituo halisi vya polisi kabla hatujaanza kujenga spesho kwa ajili ya filamu, tunabezwa filamu zetu hazina uhalisia kwakuwa selo zetu watazamaji wetu wanajua kabisa sio selo bali ni dukani kwa Mangi!
Mheshimiwa majiji kama New York, idara ya polisi (New York Police Department /NYPD) wana kitengo kipo maalum kwa ajili ya kutoa msaada kwa filamu, iwe sare, silaha, vituo vya polisi, mahakama, helikopta na hata polisi wenyewe ikitakiwa watumike na vingine vingi na kuweka polisi kadhaa katika location kufuatilia.
Mheshimiwa, New York, Los Angeles na majiji mengine huko Marekani na Ulaya nimeenda mbali, hapa jirani yetu Afrika ya Kusini hata ukikitaka kituo cha polisi wanakutajia bei ukilipa wanahamia uani mheshimiwa. Siongei mambo ya kijiweni. Nina uhakika na ninachoongea, kumbukumbu zangu za mwisho ilikuwa 2011 Afrika Kusini ukitaka helikopta ya polisi ilikuwa milioni mbili kwa saa, kumkodi polisi mmoja na sare zake ilikuwa shilingi 130,000 kwa saa. Gari la polisi ilikuwa laki mbili kasoro kidogo kwa saa. Ila pia unaweza kuomba kibali ukaweka helikopta yeyote stika ya polisi, au hata magari. Mheshimiwa, serikali ya Afrika Kusini inatoa ushirikiano wa ajabu katika filamu, cha kushangaza zaidi wizara ya viwanda na biashara wana kitengo cha kukopesha hela kwa wazalishaji ili watengeneze filamu.
Mheshimiwa waziri, serikali ya Ufilipino ikimkuta mtu na kosa la kuvaa sare za polisi (Philippines National Police /PNP) inamfunga jela miaka minne na miezi miwili, lakini waigizaji wameruhusiwa kuvaa sare hizo katika kazi zao. Mgogoro umetokea hapo majuzi baada ya muigizaji kuigiza akisaula sare hizo katika muziki mbele za watu, ndani ya tamthilia iitwayo ‘On the Wings of Love.’ Kwahiyo mheshimiwa, waigizaji waruhusiwe ila kwa masharti maalum kama walivyofanya PNP Ufilipino.
Mheshimiwa, sisemi kila muigizaji au kampuni ya uzalishaji iwe na sare au silaha la hasha, iwepo kampuni itakayoaminiwa na serikali au kitengo katika wizara yako ambacho kitakuwa na mamlaka ya kumiliki silaha, sare za polisi trafiki na kadhalika ambapo wazalishaji watakuwa wanaenda kukodi kwa gharama nafuu na pia kinasimamia maeneo ambayo vifaa hivyo vinatumika. Vitu hivyo vinaonekana ni vitu vidogo lakini ukweli hufanya filamu ziwe na msisimko wa kipekee.
Mheshimiwa waziri, serikali ikisema kurasimisha tasnia ya filamu isimaanishe kukusanya kodi tu peke yake, bali dhamira kuu iwe kuinua filamu na kodi itapatikana, maAna hata hizo stika za TRA imekuwa ni tisha toto tu maana wezi wapo wengi na wanajua stika zimewekwa kwa mikwara hakuna anayezifuatilia. Tangu tasnia irasimishwe filamu ndio hamna biashara kabisaaa afadhali hata kabla.
Kazi ya kufanya filamu ziuzike na wahusika tunufaike na serikali ipate kodi yake ni kazi ndogo mno, ilimradi serikali iamue tu mheshimiwa. Naomba wizara yako iamue sasa ili tunufaike na uwezo wetu tuliopewa na mwenyezi Mungu.
Nawapa pole Orijino Komedi kwa matatizo yaliyowakuta, lakini nashukuru pia maana imekuwa ni njia moja wapo ya kulizungumzia na kulipa umakini jambo hili, kama kifo cha Kanumba kilivyotuumiza lakini ikawa ni njia iliyofanya serikali istuke na igundue nguvu ya sanaa katika jamii.
Mheshimiwa naomba uwasaidie vijana wa Orijino Komedi wasamehewe na uliweke sawa jambo hili, tunataka sare, silaha, vituo vya polisi, mahakama, kufunga mitaa wakati tunashuti barabarani na mambo mengine mengi.Mheshimiwa kuigiza vizuri hakupeleki sanaa ya filamu kokote kama hakuna vitu vya uhalisia ndani ya filamu hizo.
Nashukuru kwa kutumia muda wako kusoma waraka huu mheshimiwa waziri, kwa uchapakazi wako nina imani tasnia yetu ya filamu itafika mbali kwa wakati huu ambapo ipo katika mikono yako. Asante.
No comments:
Post a Comment