Lipumba atibua, ngumi zatawala uchaguzi wa mwenyekiti CUF
NDANI na nje ya Ukumbi wa Mkutano unaotumiwa na Chama cha Wananchi (CUF) katika Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo jijini Dar es Salaam kufanya uchaguzi wa viongozi wa chama hicho kuna patashika, anaandika Charles William.
Nje ya ukumbi, wafuasi wa Prof. Lipumba na wale wasiomtaka wananyukana makonde. Hali ni tete.Wajumbe wa mkutano huo walio ndani, wanaendelea na upigaji kura, baadhi yao wametoka nje – wamesusa.
Ni Mkutano Mkuu wa CUF uliotanguliwa na Baraza Kuu la Uongozi (BKUT) la chama hicho lililopitisha majina matatu ya kuwania nafasi ya uenyekiti iliyoachwa na Prof. Lipumba baada ya kujiuzuli Agosti mwaka jana. Hivi karibuni kiongozi huyo aliomba kurejea kwenye nafasi yake ya uenyekiti bila mafanikio.
Prof. Lipumba na sehemu ya kundi lake bado wamo ndani, zogo kubwa linaendelea huku uamuzi wa kujadiliwa kwa barua ya kiongozi huyo aliyoomba kujuzulu ukiendelea.
Uamuzi wa kupiga kura ikiwa ni hatua ya kuamua kwamba, barua yake iridhiwe (kujiuzulu) ama la ndio unaofanyika kwa sasa.
Tangu kuwasili kwa Prof. Lipumba, hofu ndani ya ukumbi huo ilianza kutawala kwa kuwa, hakutegemewa kuwasili.
Prof. Lipumba, alivamia mkutano huo na kundi lake akidai, anasubiri mjadala wa maombi ya barua yake ya kujiuzulu uenyekiti aliyomwandikia katibu wa mamlaka ambaye ni Maalim Seif Shariff Hamad.
Hatua ya Prof. Lipumba ya kuvamia mkutano huo imetibua taratibu zote zilizokuwepo, ndani ya ukumbu huo kumeonekana sura ambazo awali hazikuwa zimezoeleka machoni mwa wajumbe wa mkutano huo.
Hatua ya Prof. Lipmba kuvamia mkutano huo inakuja ikiwa ni baada ya majina matatu ya wanachama wanaowania nafasi ya uenyekiti wa CUF tayari yametajwa.
Wanaotajwa kwenye majina hayo ni Twaha Issa Taslima, wakili wa Mahakama Kuu, Abubakar Khamis Bakary na Severine Mwijage.
Majina hayo yamepitishwa naBKUT lililoketi jana kujadili majina ya waombaji tisa yaliyofikishwa mbele ya mkutano mkuu maalum wa leo.
Kwa muda mrefu, ndani ya CUF kumekuwepo na makundi mawili makuu, moja likimtaka Prof. Lipumba na lingine likitaka atoswe.
Prof. Lipumba anadai kutumia Katiba ya mwaka 1992 Toleo 2013 Ibara ya 117 inayoeleza kwamba, “… kama hakuainisha tarehe ya kujiuzulu kwake basi mara baada ya katibu wa mamlaka iliyomteua ama kumchagua kupokea barua hiyo na kumjibu.”
Maombi ya Prof. Lipumba kujiuzulu yalimfikia katibu wa mamlaka (Maalim Seif) na kwamba, kwa mujibu wa ibara hiyo, alipaswa kupeleka maombi hao katika Mkutano Mkuu wa chama hicho kuijadili barua hiyo na baadaye kujibu barua hiyo jambo ambalo mpaka sasa halikuwa limefanyika.
Prof. Lipumba aliteuliwa kutwaa nafasi hiyo na Mkutano Mkuu mwaka 1999, hata hivyo Ibara ndiyo inayoipa mamlaka mkutano huo kukubali ama kukataa kujiuzulu kwake.
Baadhi ya wanachama ambao ni kundi lake wamekuwa wakipaza sauti wakidai ‘bado ni mwenyekiti halali’ wakitaja kifungu hichocha Katiba ya chama hicho.
Mvutano wa CUF ulidhihiri miezi michache iliyopita kwenye kongamano lililoandaliwa na Kata ya Makurumla Manispaa ya Kinondoni ambapo wajumbe waliibua hoja ya ukimya wa taarifa kuhusu maombi ya kujiuzulu ya Prof. Lipumba.
Katika kongamano hilo, Mohamed Mgomvi, mmoja wa wanachama wa CUF alisema, upande wa bara chama hicho kimebaki kwenye uyatima akidai hakuna mtu madhubuti anayeweza kukiendesha kama Prof. Lipumba.
“Nashangaa viongozi wetu mnasema habari zisizoeleweka juu ya kujiuzulu kwa Lipumba badala ya kusema ukweli nini kinaendelea huko ndani, tangu alipoondoka Lipumba hakuna maendeleo alafu mnasema tupo pamoja naye, haiingii akilini hata kidogo,” alisema.
Maganga Dachi, mwanachama wa CUF katika mkutano huo pia alisema, kwa mujibu wa Katiba ya CUF, barua ya kujiuzulu inatakiwa ifike katika Mkutano Mkuu uliomchagua jambo ambalo halijafanyika.
“Kwa hatua hiyo chama kinavunja Katiba maana hadi leo hakuna kinachoendelea kama hivyo suala la Lipumba, linatakiwa kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu nasi tunamtaka Lipumba arudi katika nafasi yake ili chama kiendelee na shughuli za kimaendeleo,” alisema Dachi.
Tutawaletea matokeo ya uchaguzi huo punde baada ya kutangazwa….
No comments:
Post a Comment