NSSF Yaburuzwa Mahakamani

MATANGAZO

MATANGAZO

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limeburuzwa mahakamani na wakazi 87 waliokopeshwa nyumba za mradi wa shirika zilizoko Kijichi jijini Dar es Salaam, wakiiomba lisiwabugudhi hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa. 

 Kesi hiyo imefunguliwa na wakazi hao katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, wakilalamikia Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF na Kampuni ya Majembe Auction Mart. Kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana mbele ya Jaji Penterine Kente. 

 Wakili wa walalamikaji hao, Benito Mandele, amewasilisha maombi mahakamani hapo kutaka itoa amri ya kutokubugudhiwa na mazingira ya makazi hayo yabaki kama yalivyo hadi kesi yao ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi. 

Katika kesi ya msingi, mbali na NSSF, mlalamikiwa wa pili ni Majembe ambaye hakufika mahakamani. Wakili Mandele alidai kuwa alipeleka wito wa mahakama katika ofisi yake iliyoko Mwenge, lakini hakufanikiwa kumpata kwa kuwa amehamisha ofisi eneo hilo. 

Jaji Kente alisema mahakama inatoa hati nyingine kwa ajili ya mlalamikiwa wa pili ili afike mahakamani kusikiliza kesi dhidi yake. Kesi ya msingi itasikilizwa Oktoba 17, mwaka huu, na maombi ya kutokubughudhiwa yatasikilizwa Agosti 24, mwaka huu.

Wakazi hao kupitia kwa wakili wao, waliamua kukimbilia mahakamani kufungua shauri hilo, baada ya kushindwa kupata ufumbuzi wa madai yao katika Taasisi ya Usuluhishi kutokana na walalamikiwa kutofika. 

Ilidaiwa kuwa wakazi hao waliamua kwenda katika taasisi ya usuluhishi kutokana na mkataba wao kuwataka kufanya hivyo kabla ya kuamua kwenda mahakamani. 

Kwa mujibu wa hati ya madai, wakazi hao wanadai kwamba mlalamikiwa wa kwanza (Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF), ameshindwa kutekeleza makubaliano kwa mradi huo kukosa huduma za kijamii. 

Aidha, wanadai nyumba hizo hazina ubora hali iliyowalazimu wengi wao kutumia fedha zao kufanya ukarabati. 

Wanadai kuwa kutokana na hali hiyo, baadhi ya wakazi wameshindwa kulipa fedha ambazo wanatakiwa kulipa kila mwezi, hivyo Majembe walifika na kuwapatia notisi na kuwatangazia kuwaondoa. 

Wakazi hao wanaiomba mahakama hiyo, kuiamuru bodi hiyo kurejea mikataba, kutambua majukumu ya msingi ya kila upande na nyumba ziwe za kuwawezesha kuishi na kuwe na huduma za kijamii. 

Katika maombi, wakazi hao wanaiomba mahakama hiyo kutoa amri ya hali ilivyo kwa wakazi hao katika makazi hayo ibaki kama ilivyo mpaka kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.