Waziri Mkuu Awaweka Sawa Watumishi Wa Ofisi Yake, Tayari Kwa Safari Ya Dodoma

MATANGAZO

MATANGAZO
Waziri Kassim Majaliwa amesema safari ya kuhamia Dodoma imeiva na amewataka watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wajipange kisaikolojia.

Ametoa kauli hiyo leo Agosti 18, 2016 alipokutana na kuzungumza na watumishi wa ofisi yake kutoka taasisi, idara na vitengo mbalimbali waliopo Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amewataka watumishi hao watambue kuwa uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.

“Tangu wakati huo kumekuwa na juhudi mbalimbali zilizofanyika ili kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” amesema.

“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” amesema.

“Napenda kuwatoa hofu, mambo yanaenda vizuri ila mtambue kuwa safari imeiva sasa. Kikubwa ni kwamba tutakwenda kwa awamu kama ambavyo imepangwa,” amesema.

Amewataka watumishi hao wazidishe mshikamano miongoni mwao huku wakitambua kuwa wana dhamana ya kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na uaminifu.

“Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu tunapaswa tutambue dhamana tuliyonayo. Tufanye kazi kwa bidii. Tuhakikishe kila kilichopangwa kinafanyika kwa ufanisi na kinafanikiwa,” amesema.

Julai 25 katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa, Waziri Mkuu aliwataka mawaziri wote kuhamia Dodoma mara moja na kusema kuwa yeye atakuwa wa kwanza ifikapo Septemba.