Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Atembelea Kijiji Cha Katumba Wilayani Mpanda,azindua Mnara Uliojengwa Na Wakimbizi Waliopewa Uraia Wa Tanzania
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa wakimbizi waliopewa uraia wa Tanzania na kuitumia vibaya nafasi hiyo kwa kuingiza watu wengine kinyume cha sheria watanyang’anywa na kurudishwa walikotoka.
Aidha, Waziri Mkuu amewaomba viongozi wa dini wawe wanawaelimisha waumuni wao umuhimu wa kulinda amani na kuishi kwa kufuata sheria na taratibu za nchi husika.
Kauli hiyo imetolewa jana (Jumapili, Agosti 20, 2016) na Waziri Mkuu wakati akizungumza na waliokuwa wakimbizi wa Burundi ambao kwa sasa wamepewa uraia wa Tanzania wanaoishi katika Kata ya Katumba, Halmashauri ya Nsimbo wilayani Mpanda.
“Wakimbizi waliopewa uraia wameendelea kuingiza ndugu zao. Naagiza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ifanye ukaguzi katika kambi zote kwa sababu zimegeuzwa kuwa maficho ya kuwahifadhi watu wanaoingia nchini bila ya vibali,” alisema.
“Hakikisheni mnachukua hatua kwa wote watakaoingiza watu kinyemela katika kambi za wakimbizi za Mishamo na Katumba. Pia msiruhusu watu kuleta silaha kwenye maeneo haya. Tanzania watu wanaoruhusiwa kutembea na silaha ni askari tu,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alisema lazima ulinzi uimarishwe katika maeneo ya mipakani na wasipofanya hivyo watu wengi wataingia nchini bila ya kuwa na vibali hivyo kusababisha ongezeko kubwa la idadi ya watu.
Wakati huo huo Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda wasiwaudhi wakulima na wafanyabiashara wadogo kwa kuwatoza ushuru kwenye mazao wanapotoka shambani kama debe moja la nafaka na wanaouza bidhaa ndogo ndogo.
“Mkulima ametoka shambani na debe moja la mahindi unamtoza ushuru maana yake nini? Halmashauri tusitafute mgogoro katika hili. Tafuteni biashara za kutoza ushuru, mkulima anatoka kijiji cha Kanoge anakwenda kijiji cha Ikongo ushuru wa nini?" Waziri Mkuu alihoji.
Waziri Mkuu alisema “Tumewasisitiza mkusanye kodi lakini siyo hivyo. Mkiendelea kutoza ushuru kwa wakulima wanaotoka shambani na mahindi kidogo mtasababisha wakate tamaa ya kulima,”.
Akisoma taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Katavi jana jioni (Jumamosi, Agosti 20, 2016) mara baada ya Waziri Mkuu kuwasili mkoani hapa Mkuu wa mkoa, Meja Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga alisema mkoa una jumla ya wakimbizi 6,918 wanaoishi katika kambi za Mishamo na Katumba ambapo kati yake wakimbizi 2,150 waliomba uraia wa Tanzania na kunyimwa.
Alisema wakimbizi 2,489 walichagua kurejea nchini kwao Burundi ila bado wapo katika kambi hizo huku wengine 653 waliomba uraia lakini majina yao hayakuonekana kwenye orodha ya waliokubaliwa wala kukataliwa uraia hivyo mkoa unaendelea kufuatilia ili kujua hatma yao.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa wakimbizi wengine sita walichagua kubaki nchini lakini hawakuomba uraia, 398 waliomba uraia ila fomu zao hazikukamilika,249 waliomba uraia ila majina yao hayakurudi huku wengine 973 hawakusajiliwa walipoingia nchini mwaka 2007/.2008.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, AGOSTI 21, 2016.
No comments:
Post a Comment