Baba Mzazi: 'Abdul Nondo babu yake ni muasisi wa TANU'

MATANGAZO

MATANGAZO
Abdul Nondo, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye anakabiliwa na kesi ya kujiteka mwenyewe, mzazi wake Omar amethibitisha kuwa baba yake alizaliwa mwaka 1919 huko Ujiji, Kigoma na kuwa ni miongoni mwa waasisi wa chama cha Tanu.

Mzee Omar, alisema baba yake huyo aliyemtaja kwa jina la Omar Kagobe alipata watoto 30, mmoja akiwa yeye.

“Nashangaa hao wanaomkamata na kumhoji mtoto wangu kuwa sio raia, wananichekesha sana kwa kuwa najua mwisho wa siku watajua ukweli wake. Ukweli ni kwamba wazazi wangu ndio waasisi wa Tanu na walishiriki kikamilifu katika kupigania uhuru wa nchi hii, hivyo suala hilo halinipi wasiwasi wala hofu na hivyo vyeti wanavyovitaka mbona vipo tu, ila waelewe kuwa sisi ni Wamanyema halisi na ni raia halali wa nchi hii,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa ACT - Wazalendo, Mkoa wa Kigoma, Sendwe Mbaruku, alitoa taarifa Alhamisi kuhusu suala la Nondo kuhojiwa na uhamiaji na kusema; “Kijana Abdul ni mtoto wetu hapa Kigoma, wazazi wake ni wakazi na wapiga kura wa hapa Ujiji, zaidi ni Watanzania wenzetu.”

Maelezo haya yametolewa na mzazi huyo Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu uraia wake.

Mzazi huyo amesema babu yake Nondo, alishawahi kuwa Polisi kwa miaka 18 kuanzia mwaka 1940 hadi 1958 na alishafanya kazi huko Mabatini mkoani Mwanza na sehemu nyingine za nchi.

Alisema babu yake wakati akiwa polisi, ndipo zilipoanzishwa Kota za Msimbazi, Dar es Salaam na jina lake lilikuwa maarufu, akijulikana kama Mzee Kagobe.

Kama haitoshi alisema bibi yake Nondo alikwenda kuhiji, mnamo 1970 na alipewa hati ya kusafiria ya Tanzania, huku akihoji, “Kama angekuwa sio raia wa Tanzania angepewaje hati hiyo?”

Baada ya Nondo kuripoti polisi mjini Mafinga alishikiliwa na jeshi hilo Mkoa wa Iringa na baadaye kukabidhiwa kwa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema kupitia uchunguzi wa kisayansi, wamebaini kuwa hakuwa ametekwa, bali alijiteka na tayari suala lake lipo mahakamani, Iringa.