Mwanza: Mtendaji Atupwa Jela Miaka 30 kwa Kulawiti na Kubaka

MATANGAZO

MATANGAZO
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela na faini ya Sh800,000 ofisa mtendaji wa Kata ya Mkuyuni jijini hapa, James Chorangirwe baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka na kumlawiti mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka 12.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na hakimu mkazi mfawidhi mwandamizi wa mahakama hiyo, Wilbert Chuma baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka. Upande wa mashtaka ulidai mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kati ya Novemba 14 hadi 16, 2016.

Kwa mara ya kwanza, shauri hilo namba 239/2016 lilifunguliwa mahakamani Novemba 11, 2016 katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana ambapo hakimu aliyekuwa anasikiliza alijitoa baada ya kuwepo madai ya kupanga njama za kuharibu kesi.

Baada ya kuwepo madai hayo, Januari 2018, Rais John Magufuli aliingilia kati kwa kumuagiza mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kufuatilia kwa karibu upelelezi, uendeshaji na hatima ya shauri hilo ili haki iweze kutendeka.

Januari 18, 2017, Mongella alitembelea Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou-Toure alikokuwa akitibiwa mtoto huyo ambapo aliusoma hadharani mbele ya waandishi wa habari na watumishi wa hospitali hiyo ujumbe mfupi wa simu alioandikiwa na Rais Magufuli kuhusu suala hilo. Katika ujumbe huo, Mongella aliwataja baadhi ya watendaji, maofisa wa polisi (majina yao yanahifadhiwa kwa sasa) ambao walituhumiwa kula njama za kuhujumu upelelezi na mwenendo wa shauri hilo.