RC Gambo Amtoa Hofu Rais Magufuli Kuhusu Maandamano ya Mange Kimambi
Mkuu  wa Mkoa wa Arusha Mrisho gambo amemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutotishwa na maandamano ya mitandaoni  yanayoratibiwa na Mange Kimambi, kwani mkoa wa Arusha uko salama.
Mrisho  Gambo ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salam zake kwa Rais Magufuli,  kwenye sherehe za uzinduzi wa nyumba za polisi mkoani Arusha, kwenye  uwanja wa Sheikh Amri Abedi.
Kwenye  salamu hizo Mrisho Gambo amesema mkoa wa Arusha ni salama na wakazi wa  Arusha hawana haja ya maandamano, kwani wanachohitaji ni uongozi wake  ambao unawaletea maendeleo makubwa.
Mrisho  gambo aliendelea kwa kueleza kuwa anatambua kazi ya kubwa aliyonayo  Rais ya kupigana vita ya uchumi, na watu wengi wasiopenda nchi hii  watachukia kutokana na hilo.
“Mheshimiwa  Rais nikuhakikishie tu Arusha ni salama, wala usitishwe na mbwembwe za  kwenye mitandao, watanzania halisi ni hawa hapa wenye Arusha yao. 
"Watanzania  wa Arusha wamechoka na maandamano, wanataka uongozi wa kwako ambao  unawaletea maendeleo. Ninajua vita uliyokuwa nayo ni kubwa sana, Mwl.  Nyerere alikuwa na vita ya ukombozi, akaimaliza salama, 
"Mheshimiwa  Rais vita yako wewe ni ya kiuchumi, ni vita inayopigana na mabeberu  ambao wanawatumia wengine kukwamisha jitihada zako. Watu wengi ambao  hawaitakii mema nchi hii hawawezi kuipenda”, amesema Mrisho Gambo.
Sambamba  na hilo Mkuu wa mkoa huyo wa Arusha amemshukuru Rais Magufuli na wadau  kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba hizo za askari polisi, ambazo awali  ziliteketea kwa moto.

No comments:
Post a Comment