Waziri Mkuu: Serikali Kuimarisha Masoko Ya Mazao Makuu Matano
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha vyama vya msingi vya ushirika vya mazao ya kilimo na masoko vinavyozalisha mazao ya kimkakati ya biashara ya pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku.
Amesema katika mwaka 2018/2019, Serikali inalenga kuimarisha masoko ya mazao hayo kwa kuhamasisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo mazao hayo yatazalishwa na kuuzwa kupitia vyama vya ushirika kwa njia ya minada.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) Bungeni mjini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019 kwenye mkutano wa 11 wa Bunge.
Waziri Mkuu amesema pamoja na hatua hizo, Soko la Bidhaa ambalo limeshaanzishwa, litasaidia sana kuimarisha masoko ya mazao kwani yatakuwa yanauzwa kwa njia ya ushindani mkubwa huku wakulima wanaozalisha kwa ubora wakinufaika na bei ya juu zaidi.
“Serikali imeamua kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao matano ya biashara ambayo ni chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku. Lengo ni kuongeza mapato ya wakulima, kuwa chanzo cha kuaminika cha malighafi katika uchumi wa viwanda, na kuendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira na fedha za kigeni.
Amesema uamuzi wa kuongeza usimamizi katika uzalishaji wa mazao hayo makuu ya biashara unatokana na ukweli kwamba, kwa kipindi kirefu uzalishaji ulishuka kutokana na changamoto kadhaa.
“Miongoni mwa changamoto hizo ni kupungua tija katika uzalishaji, baadhi ya wakulima kuacha kulima mazao hayo kutokana na kukata tamaa kwa sababu mbalimbali zikiwemo vyama vya ushirika kutotekeleza vema wajibu wao, wizi, dhuluma na pia ushiriki mdogo wa maafisa kilimo katika kusimamia kilimo cha kitaalamu,” alisema.
Alizitaja sababu nyingine za kushuka uzalishaji wa mazao hayo kuwa ni huduma zisizoridhisha za ugani na utafiti, ukosefu wa pembejeo bora, utitiri wa tozo na wingi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika.
Akitolea mfano, Waziri Mkuu alisema uzalishaji wa pamba ulipungua kutoka tani 456,814 mwaka 2013/2014, hadi tani 282,809 mwaka 2015/2016. Kwa upande wa tumbaku, Waziri Mkuu alisema uzalishaji katika kipindi cha miaka minne ulishuka kutoka tani 126,624 mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani 60,929 mwaka 2015/2016.
“Serikali imechukua hatua za kuimarisha utawala bora kwenye vyama vya ushirika kwa kusimamia chaguzi za vyama 2,537, chaguzi za viongozi wa bodi za vyama vya ushirika 532 na kufanya kaguzi katika vyama vya ushirika 2,896 vikiwemo vyama vikuu. Kazi za kusimamia vyama vya ushirika zinaendelea,” alisema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alisema Serikali inasimamia uendelezaji wa mazao hayo moja kwa moja kupitia maafisa kilimo na Bodi za Mazao na kwamba imechukua hatua za kufuta baadhi ya tozo zilizokuwa kero katika mazao makuu ya biashara pamoja na kuhakikisha kwamba mauzo yanafanyika kwa njia ya wazi na inayoleta ushindani.
“Kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali kusimamia mazao makuu ya biashara, tayari tumeanza kuona matokeo chanya kwa kuongezeka uzalishaji wake. Kwa mfano, hadi mwezi Machi 2018, uzalishaji wa mazao ya asili ya biashara ulifikia tani 804,025. Uzalishaji huu unaashiria ongezeko la mavuno ikilinganishwa na mwaka 2016/2017. Ongezeko hilo la uzalishaji wa mazao ya biashara linakwenda sambamba na kuimarika kwa mwenendo wa bei za mazao hayo hususan korosho na kahawa,” alisema.
Waziri Mkuu aliliomba Bunge likubali kupitisha sh. 143,618,762,698 zikiwa ni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2018/2019 ambapo sh. 74,527,321,698 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 69,091,441,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile, Waziri Mkuu aliliomba Bunge liidhinishe sh. 125,521,100,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 117,205,487,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 8,315,613,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO, APRILI 4, 2018
No comments:
Post a Comment