Polisi Yadai Kukerwa na Wasanii wa Orijino Komedi Kukatikia Viuno Sare za Jeshi Hilo.........Masanja Mkandamizaji Aendelea Kusakwa

MATANGAZO

MATANGAZO

WAKATI mwigizaji wa kundi la Orijino Komedi, Emmanuel Mgaya 'Masanja Mkandamizaji' akiendelea kusakwa, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema unenguaji uliofanywa na wasanii wa kundi la Orijino Komedi jukwaani wakiwa wamevalia sare za jeshi hilo ndiyo sababu ya kuwakamata.

Juzi usiku jeshi hilo liliwatia mbaroni waigizaji wanne wa kundi hilo kwa kosa la kuvaa nguo zinazodhaniwa kuwa ni za Jeshi la Polisi kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

Waliokamatwa Jumanne na kuachiwa kwa dhamana juzi ni Lucas Lazaro (Joti), Serious David, Alex John na Isaya Gideon.

Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna Hezron Gyimbi, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema kitendo hicho cha kunengua mauno kilidhalilisha jeshi hilo na waliwakamata ili kuwahoji na pindi watakapobaini uhalali wa sare hizo, watawachukulia hatua zaidi za kisheria.

“Waigizaji hawa wa komedi tumewaita ili kuwahoji kufahamu uhalali wa sare walizokuwa wamezivaa ambazo zinafanana na za jeshi hili, kinyume cha sheria za nchi.

“Lakini kama mlivyoona mkanda waliokuwa wamevaa, una tofauti gani na huu niliovaa?” alihoji Naibu Kamishna Gyimbi huku akionyesha mkanda wake.

Alisema jeshi hilo lina miiko na kanuni zake, na hawaruhusiwi kushiriki shughuli za sherehe na kucheza wakiwa wamevalia sare hizo.

“Siyo Jeshi la Polisi tu, hata wengine; Magereza au JWTZ (Jeshi la Wananchi la Tanzania) huruhusiwi kuvaa sare zao bila kibali maalum labda cha kutaka kuelimisha jamii… lakini hawa hawakuwa na kibali na walivaa wakiwa kwenye shughuli ya mwenzao,” alisema.

Naibu Kamishna huyo Gyimbi alisema jeshi hilo linaendelea kumsaka Masanja kwa kuhusika kwenye tukio hilo likiamini ni mshiriki anayeweza kufahamu walikozipata sare hizo.

Alisema Masanja ambaye hakuvaa sare hizo wakati wa sherehe hiyo ya mapokezi ya harusi yake, pia alishiriki kwenye shughuli hiyo, hivyo wanataka kumhoji wakiamini ana ushahidi wa tukio hilo.

"Masanja tunamtafuta kama mhusika wa shughuli hiyo ambayo waigizaji wenzake walivaa sare zinazodhaniwa kuwa ni za Jeshi la Polisi kinyume cha sheria na taratibu za nchi,” alisema.

Aliongeza kuwa Masanja anatakiwa kujisalimisha polisi na watamkamata mahali popote atakapopatikana.

Video za waigizaji hao wakiwa na nguo zinazodaiwa na Jeshi la Polisi kuwiana na sare zao, zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonyesha wakitoa burudani kwenye harusi ya Masanja.

Masanja alifunga ndoa, Jumapili iliyopita na waigizaji hao burudani kwenye tafrija ya kupongeza maharusi.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea na mwandishi wa gazeti la Mwanahalisi na Mseto, Josephat Isango jana waliripoti kituoni hapo kwa ajili ya kuitikia wito wa jeshi hilo.

Agosti 15, Kubenea aliripoti kituoni hapo na kuhojiwa juu ya makala iliyochapishwa kwenye gazeti la Mwanahalisi, wiki tatu zilizopita ikielezea hali ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu Zanzibar.

Isango naye aliripoti kituoni hapo na kuhojiwa kuhusu habari aliyoiandika kwenye gazeti la Mseto lililofungiwa kwa miezi 36 na serikali wiki iliyopita.

Isango aliandika habari kwenye gazeti la Mseto la Agosti 4 hadi 10 yenye kichwa cha habari 'Waziri amchafua JPM'.
Wote wawili walirudi kuendelea na shughuli zao na Isango alitakiwa kurudi leo, wakati Kubenea hakupangiwa siku ya kurudi.