Tanzania, Israeli Zakubaliana Kuinua Sekta Za Maji Na Umwagiliaji Nchini

MATANGAZO

MATANGAZO
Serikali za Tanzania na Israeli zimekubaliana kuinua Sekta za Maji na Umwagiliaji kwa kuweka mikakati madhubuti, ili kuleta mapinduzi katika sekta hizo nchini katika kufanikisha lengo la taifa la kuwa na uchumi wa viwanda.

Makubaliano haya yalifikiwa jana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge na Balozi wa Israeli nchini, Yahel Vilan katika mazungumzo yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Ubungo Maji, baada ya Balozi huyo kutembelea wizara hiyo.

"Tunapenda kushirikiana na Serikali ya Israeli kwa kupata utaalamu wa kutoa huduma ya majitaka na jinsi ya kuyatibu na kuyatumia kwa matumizi mengine, ambayo kwa sasa ni moja ya changamoto kubwa, ikizingatiwa ongezeko la huduma ya majisafi inaambatana na ongezeko la majitaka na kufikia mwaka 2020 ni lazima tuwe tumefanikiwa katika jambo hilo", alisema Mhandisi Lwenge.

Waziri Lwenge aliendelea kusema Tanzania pia ingependa kuwa na ushirikiano na Israeli kwenye kilimo cha umwagiliaji, lengo ni kuhakikisha Tanzania inaongeza eneo linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,326 za sasa mpakakufikia hekta 1,000,000. 
Vilevile, kuhifadhi maji kwa kujenga mabwawa na matumizi ya maji yaliyo chini ya ardhi kwa ajili ya umwagiliaji kwenye maeneo yenye changamoto ya maji kama Dodoma, Katavi na Singida ili kuwepo chakula salama na cha kutosha nchini.

Katika mazungumzo hayo Balozi Vilan alisema maji ni moja ya kipaumbele katika maeneo ya ushirikiano wao na Tanzania. 
Na Israeli iko tayari kuisadia Tanzania kwenye suala la majitaka, kwani ni taifa linaloongoza duniani kwa huduma ya kutibu majitaka, zaidi ya asilimia 85 ya majitaka hutibiwa na kutumika tena kwa matumizi mbalimbali. Hivyo, wako tayari kwa kushirikiana na Tanzania katika jambo hilo.

"Israel piaipo tayari kuwajengea uwezo watanzania katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji,kwa kwenda kujifunza Israeli tunavyofanya na jinsi tulivyopiga hatua kubwa katika sekta hiyo.  
"Nina hakika ndani ya miaka kumi ijayo Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta hii, kwa kuwa ina maji ya kutosha, ardhi ya kutosha na hali ya hewa ni nzuri kwa kilimo," alisema Balozi Vilan.

Hii ni sehemu ya ziara ya Balozi wa Israeli nchini ya kutembelea wizara mbalimbali Tanzania kwa lengo la kukuza ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.