Waziri Mkuu: Ukaguzi wa Wanafunzi HEWA Ufanyike Nchi Nzima

MATANGAZO

MATANGAZO
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu nchini wafanye ukaguzi katika shule ili kubaini wanafunzi hewa kwenye mpango wa elimu bure.

“Kila mwezi Serikali inapeleka shule zaidi ya shilingi bilioni 18 kugharamia elimu bure na sasa tumeanza kuona udanganyifu katika sekta ya elimu kwa kuwa na wanafunzi hewa. Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu nendeni mkafanye ukaguzi ili mpate takwimu sahihi,“ amesisitiza.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Alhamisi, Agosti 18, 2016) alipokutana na watumishi na viongozi wa Manispaa ya Ilala katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

 “Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu mkiona takwimu ziwachanganya, ni lazima mtoke maofisini na kwenda katika shule zilizo kwenye mpango wa elimu bure mkafanye uhakiki wa idadi ya wanafunzi,” alionya.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema maamuzi yanayotolewa kwenye  vikao vya madiwani lazima yawe na tija na ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika kuboresha shunghuli za maendeleo badala ya kujilipa posho.

“Lazima mjipange vizuri na kupunguza changamoto zinazoikabili wilaya yenu. Malipo yote ni lazima yawe yale yaliyoainishwa katika waraka na si vinginevyo.Mtu wa Ilala unadai nauli ya sh. 200,000; hivi unakuwa unatoka wapi hata mimi wa Lindi silipwi nauli hiyo,” alihoji.

Waziri Mkuu alisema ni lazima halmashauri zote nchini zizingatie sheria za Mamlaka ya Serikali za Mitaa na watendaji wake wajiulize kama mambo wanayoyafanya yana tija na wanawatendea haki watu wanaowatumikia.

Alisema Serikali inataka kuwa na watumishi wanaotambua nafasi zao na watakaofanya kazi kwa uadilifu, uaminifu pamoja na uwajibikaji mkubwa hivyo kila mtu ahakikishe anafanya kazi vizuri na yenye matokeo chanya.

“Kuna watu wanaona ukuu wa idara ndiyo kila kitu, hata yule anayekimbiza mafaili hathaminiwi, hili si jambo jema! Ninyi wote ni kitu kimoja, ni watumishi wa Serikali, hivyo kila mmoja amthamini mwenzake,” alisema.

Waziri Mkuu alisema: “Mkurugenzi yeyote asikubali kuwa na wakuu wa Idara wasiokuwa na ushirikiano na watumishi wengine kwa sababu hataweza kupata mafanikio ya kiutendaji ndani ya eneo lake,”.

 IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, AGOSTI 18, 2016.