TUMWAMBIE ARSENE WENGER SOKA IMEACHA UPUMBAVU.
Na Richard Leonce
Kilichotokea Jumapili ya Agosti 14 kimepita, sana sana tupeane pole tu kwa homa iliyotokana na kichapo kile huku tukiweka akilini ukweli kwamba tunaenda King Power kukutana na mabingwa watetezi Leicester Jumamosi ijayo.
Tulicheza mchezo wa mwisho wa kujipima ubavu dhidi ya Manchester City kabla ya kuanza ligi, mchezo ambao tulionesha kiwango kiwango kuzuri na kushinda. Baada ya kushinda, Arsene Wenger akaongea na vyombo vya habari akisema amefurahishwa na muunganiko mzuri wa timu yake na inaonekana ipo vizuri kwenye utimamu wa mwili.
Wiki moja baadae, ligi ikaanzia nyumbani kwa kichapo kizuri kutoka kwa Liverpool na moja kati ya sababu za Arsene Wenger ikawa ni timu yake kutokua tayari kwenye utimamu wa mwili kuanza ligi. Huyu ni Arsene Wenger yule yule, siyo mtu mwingine.
Najiuliza la ukweli ni lipi hapa?Tuseme ni la pili, sawa. Je ni lini Arsenal itaanza ligi ikiwa tayari? Kumbukumbu zinaonesha katika misimu saba, wameshinda mara moja tu katika mchezo ya ufunguzi. Tena mara moja yenyewe ni msimu wa 2014/15 kwa goli ambalo lilifungwa dakika za majeruhi na Aaron Ramsey dhidi ya Crystal Palace na matokeo yakawa 2-1.
Lakini ni kwa nini timu ianze ligi ikiwa haipo tayari kwa misimu yote hiyo? Ina maana hilo siyo tatizo ambalo linapaswa kushughulikiwa? Najua kwamba Arsene Wenger ni mmoja kati ya makocha kama si yeye peke yake ambaye amewahi kushauri dirisha la usajili liwe linafungwa kabla ya ligi kuanza, lakini cha ajabu ni kwamba yeye mwenyewe hupenda kusajili wachezaji wakati ligi imekwishaanza. Yaani wabantu wanasema “Zilongwa Mbali, Zitendwa Mbali.”
Ndugu zangu Arsenal ina matatizo lakini kibaya zaidi ni kwamba tumekua hatuambiwi ukweli juu ya matatizo yake, nitakupa mfano wa usajili wa huyu beki Rob Holding kutoka Bolton. Huyu Arsenal walipeleka ofa ya Pauni Milioni 1.5 wakimtaka tangu mwezi Mei lakini Bolton wakaikataa wakitaka Pauni milioni 2.5.
Arsenal wakaondoka zao, wakaenda wapi sijui wakatumia miezi miwili kuongeza hiyo Pauni milioni 1 na wakamsajili mwezi Julai. Unaweza kujiuliza kilichowachelewesha kwa muda wote huo ni huo mshahara wa miezi miwili au ni kitu gani?
Je ingetokea timu ikamuwahi huyo mchezaji ingekuaje na tayari tulishaonesha nia ya kumtaka?
Unaweza kusema katika suala la kufanya usajili kwa wakati sahihi, Arsenal inaweza kuzidiwa hata na Yanga ya Dar es Salaam. Matatizo ya Arsenal huwa yanasemwa na kila mchambuzi duniani na hata Arsene Wenger huwa anayakiri lakini anakua mgumu sana kuyatatua. Kila mmoja wetu anakumbuka na kama hukumbuki nitakukumbusha ilivyomchukua Wenger miaka 10 kukubali kwamba Nicklas Bendtner siyo mshambuliaji mwenye hadhi ya kuichezea Arsenal.
Ilivyomchukua miaka mingi kukubali kwamba Abou Diaby hatokuja kumsaidia. Ilivyomchukua miaka mingi kukubali kwamba anahitaji kiungo mkabaji. Leo hii tunasema kwamba timu inahitaji beki, unaenda sokoni kumnunua beki mdogo wa ligi daraja la kwanza. Per Mertesacker anaumia, bado unaamua kumpa Laurent Koscielny mapumziko kwa sababu ya uchovu wa Euro ambayo alicheza pamoja na akina Dimitri Payet ambao wameshaanza kuzitumikia timu zao.
Gabriel Paulista anaumia bado unasita sita kutoa pesa kusajili beki aliyekomaa. Ni lazima uanze ligi na kichapo. Mara nyingi huwa tukisema tunaambiwa hatujui kitu kuhusu ukocha, lakini kama miezi miwili iliyopita ulituma ofa ya kumsajili Jamie Vardy maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba unahitaji mshambuliaji wa kiwango chake, lakini sasa ni miezi miwili imepita tangu Arsenal imkose Vardy na haijafanya lolote kwenye nafasi ya ushambuliaji. Ina maana unaenda kuanza ligi ukiwa na mahali ambapo unakiri pana upungufu.
Nilisema kwamba huwa sipendi usajili ambao unafanyika wakati timu imekwishaanza mashindano, lakini sikusema kitu kibaya kuhusu hilo. Kibaya zaidi huwa ni kufanya usajili wakati timu imeanza mashindano vibaya. Hata kama utasajili mchezaji mzuri lakini utamfanya ajisikie mwenye gunia la misumari kichwani ambaye ameletwa kutembea juu ya maji ili timu iliyoanza vibaya ifanye vizuri.
Naona picha ile ile kwenye suala la beki Skodran Mustafi ambaye taarifa zinasema Arsenal wameshamalizana nae juu ya mshahara na mambo mengine binafsi lakini kilichobaki ni uhamisho wake tu. Valencia wamesema ana thamani ya Euro milioni 25 tu, lakini tangu waseme hivyo mambo yamekua kimya.
Mtu kama Mustafi ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Ujerumani kilichocheza fainali za Euro mwaka huu unategemea auzwe kwa bei ya chini ya hapo kweli? Nasikia tayari Arsenal wameweka machaguo mengine kama watamkosa Mustafi, lakini mimi bado sioni sababu ya kumkosa mchezaji unayemhitaji kama bei yake ni Euro Milioni 25.
Mimi niliwapenda sana vijana wetu Rob Holding na Colum Chambers kwenye mchezo dhidi ya Liverpool. Walicheza kwa uwezo wao wote lakini mwisho wa siku uwezo wao haukutosha mbele ya safu ghali ya ushambuliaji ya Liverpool.
Jinsi Roberto Firminho na Sadio Mane walivyokua wakiwapindua pindua ndivyo haswa inavyopaswa kuwa. Unategemea mshambuliaji wa Pauni milioni 30 afanye nini kwa beki wa Pauni milioni 2?
Wenger aliwabebesha mzigo mzito sana. Ni mzigo mzito kwa sababu walipaswa kupambana na maadui wawili. Adui wa kwanza ni ukubwa wa Arsenal, adui wa pili ni Liverpool. Wangeweza kufaulu kama bahati ingekua upande wao lakini haikua hivyo na soka ilishaacha huo upumbavu.
Sasa tunaenda kucheza na timu ngumu sana ya Leicester ugenini. Leicester ambayo tayari imepoteza mchezo wa kwanza kama sisi. Hii itakua ni mechi ngumu sana kuitazama na tayari Wenger ameamua kwamba atamtumia Laurent Koscielny, bila shaka na Column Chambers.
Zaidi ni kwamba Aaron Ramsey na Alex Iwobi tayari wamepata majeraha na watakua nje kwa wiki mbili mpaka tatu. Kuhusu Gabriel bado atakua nje kwa wiki sita hadi nane.Kuna mpango wa kumwongezea mkataba Serge Gnabry ambaye yupo na kikosi cha Ujerumani kinachocheza michuano ya Olympic huko Rio.
No comments:
Post a Comment