Wakala wa Jiolojia waelezea Haya Juu ya Tetemeko Bukoba

MATANGAZO

MATANGAZO
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma alisema tetemeko hilo ni kubwa kwa nusu ya kipimo cha juu cha Ritcher10 na limezidi kipimo cha chini cha ukubwa wa Ritcher tatu. Alisema limezidi lililotokea Dodoma hivi karibuni.
Profesa Mruma alisema tetemeko hilo limetokea katika mpaka wa Tanzania na Uganda, kilometa 47 kaskazini mwa Bukoba mkoani Kagera na sababu ni mpasuko wa ardhi katika Bonde la Ufa la magharibi karibu kabisa na Ziwa Victoria .
Amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwani kwa kawaida linapotokea tetemeko kubwa kama hilo hufuatiwa na matetemeko madogo na ardhi hutulia baada ya siku mbili mpaka tatu. “Kwa wakati huu ili kuepuka madhara zaidi, litakapotokea watoke nje ya nyumba na kukaa mbali na miti kwenye uwanja wa wazi na wanaoendesha magari waache mara moja,” alisema Profesa Mruma.

Alisema kwa sasa wataalamu katika kituo chao cha kupimia matetemeko cha Geita wanaendelea kupata takwimu zaidi kutokana na kuwa mpasuko wa tetemeko hilo umekuwa karibu sana na ziwa Victoria na baadaye watatoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa undani.
Waathirika wazungumza
Baadhi ya watu walioathirika kwa tetemeko hilo mkoani Kagera walilieleza gazeti hili kuwa maeneo yalioathirika zaidi mkoani humo ni Bukoba Vijijini katika Kata ya Lubale, Kitongoji cha Migala, ambapo baadhi ya nyumba zimebomoka na kupata nyufa. Pia katika Wilaya ya Muleba ni Kata ya Buganguzi.
“Tulikuwa kwenye tafrija, tukasikia nyumba nzima inatetemeka. Tulidhani ni umeme umepata hitilafu, tukakimbia nje,” alisema Berena Nkalomba, mkazi wa Kata ya Buganguzi wilayani Muleba aliyesema pia kuwa nyumba kadhaa kijijini kwao Buhanga, zimepata nyufa na nyingine kubomoka kabisa katika kata hiyo.
Mkazi mwingine wa Bukoba Vijijini, Kata ya Lubale, Mbelwa Jonathan, alisema, “Tulikimbia kutoka nje, nyumba yangu imebomoka upande.” “Hata wazee wanasema hawajawahi kushuhudia tetemeko la namna hii. Sisi tuliona vitu ndani ya nyumba vinadondoka, tukakimbilia kwenye uwanja. Tumeshuhudia nyumba zikibomoka na watu wakikimbizwa katika hospitali ya mkoa,” alisema Novert Tayebwa, mkazi wa Kashai, Bukoba Mjini.
“Ilikuwa mida ya saa tisa na nusu nikiwa nimelala ndani ndipo nikasikia mtikisiko kwa bahati mbaya nilikuwa peke yangu na nilikuwa nimejifungia ndani, lakini namshukuru Mungu maana niliweza kufungua mlango na kutoka salama,” alisema Kashura wa Bukoba Mjini.
Mkazi mwingine wa Kashai, Specioza Lukamba alisema nyumba yake pamoja na baadhi ya majirani zake wameathiriwa na tetemeko hilo. “Hapa nilipo tupo nje ya nyumba zetu…mimi nilikuwa bafuni naoga nje ya nyumba yangu, nikasikia mtetemeko, nikatoka mbio…yaani ilikuwa hali mbaya. Nyumba yangu imeharibika upande mmoja pamoja na vitu vyangu kuharibika,” alieleza Lukamba.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo alisema tetemeko hilo limetokea mkoa mzima ila taarifa walizopata ni za Manispaa ya Bukoba na kifo kimoja cha Karagwe ambapo taarifa za wilaya nyingine bado zinafuatiliwa.
Aliwashauri wananchi kuwapeleka waliopata majeraha katika zahanati zilizoko karibu nao ili wapatiwe huduma kwani dawa zimeletwa za kutosha ingawa mwanzo ziliisha na Serikali ya Mkoa ililazimika kuagiza katika Duka la dawa la MK la mtu binafsi.