‘CCM Inaongoza Uvamizi wa Viwanja Kinondoni’

MATANGAZO

MATANGAZO
MANISPAA ya Kinondoni imesema viwanja vya wazi vipatavyo 160 vimevamiwa na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaongoza katika uvamizi huo kwa asilimia zaidi ya 70.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira wa Manispaa hiyo, Mustapha Muro, alisema itafanyika operesheni kubwa   kuyarudisha maeneo hayo kwa umma.

Muro alisema katika ripoti za manispaa hiyo, Chama cha Wananchi (CUF), nacho kimevamia kwa asilimia zipatazo 2.3 na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa asilimia moja.

“Viwanja vya wazi 160 (asilimia 80) ambavyo ni mali ya manispaa vimevamiwa ingawa wapo pia watu binafsi waliofanya hivyo lakini vyama vya siasa navyo vimo.

“Manispaa tumepanga kuvirejesha katika umiliki wa umma kuanzia leo (jana) tumeanza operesheni maalumu ambayo itakuwa endelevu ya kuyapitia maeneo yote na kuyatwaa,” alisema Muro.

Alisema manispaa hiyo itasimamia operesheni hiyo kwa mujibu wa sheria ikizingatiwa inaruhusiwa kusimamia ardhi yote.

“Kwa hiyo wataalamu wetu watapita na kuweka alama na muhusika atapewa notisi ya mwezi mmoja wa kujitetea kabla ya manispaa kulitwaa eneo husika,” alisema

Alisema  jambo hilo linatekelezwa kwa kushirikisha  wanasheria wa manispaa  kuhakikisha linafanyika kwa usahihi   na kwamba ni lazima maeneo hayo yote yarudi.

Kamati hiyo ilitembelea maeneo ya kata za Makuburi    na Makurumla ambako   uvamizi umefanyika.

“Katika eneo la Makuburi watu wamevamia eneo la soko na sasa limekuwa la makazi jambo ambalo si sahihi kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Mohamed Paze ambaye ni mkazi wa eneo hilo tangu 1979, alisema eneo hilo lilivamiwa baada ya kuachwa kwa muda mrefu bila kuendelezwa.