Lipumba afanya yake mkutano wa CUF...SOMA HAPA
Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Wananchi (CUF), uliofanyika jana jijini Dar es Salaam ukilenga kuwachagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho ulivunjika baada ya wajumbe kuanza kurushiana viti na matusi baada ya kupishana katika hoja ya kumtosa aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba.
Profesa Lipumba alijiuzulu nafasi yake kabla ya kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka jana akieleza kuwa roho inamsuta kumnadi mgombea urais aliyeungwa mkono na vyama vya Ukawa. Lakini mwaka huu alirejea na kuandika barua akiomba kurejea kwenye nafasi yake hali iliyozua sintofahamu.
Taarifa kutoka ndani ya Mkutano huo zimeeleza kuwa wajumbe 832 walihudhuria lakini hoja ya kumjadili Profesa Lipumba ilipofikiwa, baadhi ya wajumbe ambao wanamuunga Mwenyekiti huyo wa zamani walizua vurugu wakipinga utaratibu uliotumika.
Baadhi ya wajumbe hao waliwaambia waandishi wa habari kuwa viongozi waliopo madarakani walifanya ubabe kwa kulazimisha kura ya kukubali au kukataa ombi la Lipumba ipigwe kwa uwazi na sio siri kama Katiba inavyoeleza.
“Haki haikutendeka, ni ubabe. Wala mkutano haikuzingatia kutimia kwa akidi. Tulilazimishwa kupiga kura kwa kunyoosha mikono wakati mazingira yaliyopo na usahihi, kura ni siri,” mmoja wa wajumbe hao alikaririwa.
Baada ya kupiga kura za wazi, Lipumba alipata kura 14 kati ya kura 832 hivyo kuonekana kukataliwa kwa kishindo, lakini vurugu zilizuka ghafla kutokana na maamuzi hayo na mkutano ukashindwa kufanikisha zoezi zima la kuwapata viongozi hao wapya.
Katika hatua nyingine, Juma Haji Duni alijiengeu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo, baada ya baadhi ya wajumbe kusisitiza kuwa katiba inamtaka mtu aliyejiuzulu na kuhamia chama kingine kusubiri miaka miwili ili agombee nafasi ya uongozi ndani ya chama pale atakaporejea.
Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mipango wa CUF, Shaweji Mketo, alisema kuwa Duni alijiondoa kutokana na maadui wa Ukawa kutaka kukihujumu chama hicho.
Mkutano huo umeahirishwa hadi utakapotangazwa tena.
No comments:
Post a Comment