Soko la Afrika Mashariki kutoingiza tena nguo za mitumba ifikapo mwaka 2018

MATANGAZO

MATANGAZO
Serikali imezimia kuachana na biashara ya kuingiza nguo za mitumba kutoka nje ya nchi ifikapo mwaka 2018.

Maazimio hayo yamebainishwa na Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama katika uzinduzi wa mafunzo ya uanagenzi ya ushonaji nguo katika kiwanda cha Tanzania Tooku Garments Company, Ltd.

Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kwamba ifikapo mwaka 2018 soko la Afrika Mashariki halitaingiza nguo za mitumba kutoka nje.
Ameongeza kuwa kwa kutekeleza azimio hilo Serikali imeandaa  mafunzo ya kuhakikisha vijana wengi wanapata stadi za kushona nguo nchini ili kuwawezesha kufanya kazi katika viwanda vilivyopo na vitakavyojengwa kwa ajili ya kutengeneza bidhaa zetu wenyewe na kuacha kutegemea bidhaa kutoka nje.

“Tumejipanga kutekeleza azimio hili na kwa kushirikiana na kiwanda hiki tunategemea kutoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 2,000 kwa mwaka katika stadi za kubuni mitindo, kukata, kushona na kumalizia nguo” alisema Mhe. Jenista.

Aidha Waziri huyo amewapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwani mafunzo hayo yatawasaidia kuendana na viwango vya soko la kimataifa na mahitaji ya soko la nguo kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kubuni mitindo, kukata na kushona nguo zenye ubora wa kimataifa.

“Imani yangu kuwa wataalamu waliopo katika kiwanda hiki watawapa ujuzi wa kutosha na wengine wataweza kupata ajira katika kiwanda hiki tumieni fursa hii mliyoipata ni ya pekee kwani mmebahatika kuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza kupata mafunzo chini ya Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini.

Mhe Jenista amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatawezesha vijana kupata ajira katika Viwanda, kujiajiri na hata kutoa ajira kwa wengine hivyo vijana watumie fursa hiyo kutengeneza mtaji na kujiunga katika vikundi vitakavyowawezesha  kufungua viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza nguo na kuendelea kukuza ujuzi waliopata.

Pia Waziri Jenista ametoa wito kwa viwanda vingine kushirikiana na Serikali kukuza ujuzi kwa vijana kupitia mafunzo ya uanagenzi na kuwahakikisha kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha Vijana kupata mafunzo ya aina hiyo.

“Napenda niwahakikishie kuwa Serikali iko bega kwa bega nanyi, fungueni viwanda vingi sehemu mbalimbali katika nchi yetu, sisi kama Serikali tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha rasilimali watu ya kuendesha viwanda hivi inapatikana”

Mbali na hayo Serikali inayo mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya viwanda na kuwa na uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Serikali iliingia makubaliano na kiwanda cha Tanzania Tooku Garments Co. Ltd kutoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 2,000 kwa mwaka katika stadi za kubuni mitindo, kukata, kushona na kumalizia nguo jumla ya vijana 1,089 waliomba nafasi ya kupata mafunzo hayo yatakayoendeshwa kwa awamu tatu na kwa sasa jumla ya vijana 430 wanapata mafunzo hayo.  Na Beatrice Lyimo-MAELEZO.