Viongozi Mbalimbali wa Chadema Waendelea Kutiwa Mbaroni Kwa Uchochezi.......Wabunge CUF Waunga Mkono UKUTA

MATANGAZO

MATANGAZO
Zikiwa zimesalia siku nne kabla ya maandamano yanayodaiwa yatafanywa na Chadema, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amekuwa kiongozi wa 26 wa chama hicho kukamatwa na polisi kwa tuhuma za uchochezi ndani ya kipindi kifupi. 

Kukamatwa kwa viongozi hao kunatokana na kauli zao zinazosisitiza kufanyika kwa maandamano yaliyopewa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), yaliyopangwa kufanyika nchi nzima Septemba Mosi. 

Hata hivyo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imezuia maandamano hayo na mikusanyiko yoyote ya kisiasa hadi mwaka 2020 kwa lengo la kuipa nafasi Serikali iliyopo madarakani kuwaletea wananchi maendeleo. 

Baadhi ya viongozi wa Chadema waliokamatwa na kuhojiwa mpaka sasa ni Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Visiwani, Salum Mwalimu, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye kesi yake iko mahakamani. 

Lissu alikamatwa Agosti 3, mkoani Singida baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Ikungi uliopo jimboni kwake kwa tuhuma za uchochezi. 

Agosti Mosi, Mbowe alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa tatu. Kiongozi huyo aliitwa kwa mahojiano maalumu kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kauli za chama hicho kukinzana na agizo la Rais John Magufuli la kuzuia shughuli zozote za kisiasa ikiwapo mikutano kufanyika nchini. 

Lema alikamatwa juzi alfajiri nyumbani kwake Njiro kwa Msola na makachero wa polisi kwa tuhuma za uchochezi ikiwa ni siku moja tangu kuachiwa kwa dhamana Diwani wa Chadema wa Kata ya Sombetini, Ally Benanga aliyefunguliwa mashtaka ya uchochezi mahakamani. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo jana alithibitisha kukamatwa kwa Lema na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea wa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi mitandaoni. 

Alisema mbunge huyo alitoa kauli za uchochezi na kuzisambaza kwenye mitandao, mapema wiki hii. 

Polisi walisema ujumbe wa Lema kwenye mtandao ulisisitiza wito wa kufanyika mikutano na maandamano ya Ukuta, kwamba Mkoa wa Arusha umejiandaa kwa lolote na yeye atakuwa mstari wa mbele. 

Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro alithibitisha kukamatwa kwa Lema na kueleza kuwa bado walikuwa hawajajua tuhuma zake. 

“Ni kweli mbunge anashikiliwa na tunaendelea kuhangaika apate dhamana leo (jana), ama afikishwe mahakamani,” alisema.

Salum Mwalimu na wenzake 17 watiwa mbaroni
Wakati Lema anakamatwa Arusha, Naibu Katibu Mkuu Visiwani, Salum Mwalimu na wenzake 17 walikamatwa wakati wakijiandaa kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mwandoya wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu. 

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 25, saa 10 jioni katika kijiji hicho. 

Lyanga alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wanajiandaa kufanya mikutano ya hadhara yenye lengo la uchochezi. 

Alisema baada ya kupata taarifa kutoka katika vyanzo vyao, walifika eneo la tukio na kuwakamata kwa kuwa hata kibali cha kufanya mkutano hawakuwa nacho.

Jana, Mwalimu na wenzake walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi na kusomewa mashtaka ya kuwashawishi wananchi kufanya vitendo viovu na uchochezi. 

 Viongozi hao walinyimwa dhamana na kurudishwa rumande hadi Agosti 30. 

Agosti 23, Diwani wa Chadema, Kata ya Sombetini, Ally Bananga (40), alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kujibu tuhuma za kuhamasisha uchochezi. 

Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi Augustino Rwezire, diwani huyo alidaiwa kuhamasisha wananchi kufanya maandamano yasiyo halali, Septemba Mosi. 

Diwani huyo alifikishwa mahakamani hapo Agosti 23, ambapo Wakili wa Serikali Charles Kagirwa, alidai alitenda kosa hilo Agosti 13, wilayani Karatu Mkoa wa Arusha. 

Pia, alisema kuwa siku ya tukio Bananga akiwahutubia wananchi katika mkutano wa wazi uliofanyika eneo la Hosteli ya Karatu, aliwahamasisha wananchi hao washiriki katika kusanyiko lisilo halali Septemba Mosi. 

Agosti 25, viongozi wengine wanne wa Chadema Jimbo la Kigoma Mjini, walikamatwa na polisi wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya uchochezi. 

Waliokamatwa ni mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Kigoma, Ally Kisala, Katibu wa Baraza la Vijana Chadema Mkoa (Bavicha), Omary Gindi, Katibu wa chama jimbo la Kigoma mjini, Frank Ruhasha na Mwenyekiti wa mtaa wa sokoni katika Kata ya Katubuka, Moses Bilantanye. 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (DCP), Ferdinand Mtui alikiri viongozi hao wanne kushikiliwa kituoni hapo kwa muda lakini walipata dhamana, hivyo kuruhusiwa kuondoka na kutakiwa kuripoti kituoni hapo jana. 

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Shaaban Madede aliwaomba Polisi kwamba chama hicho kimejipanga kuandamana kwa amani na kufanya mikutano kila pembe ya mkoa, lengo ikiwa ni kufikisha ujumbe kwa wananchi juu ya kilio chao dhidi ya Serikali kukandamiza demokrasia. 

Wabunge CUF  Waunga Mkono UKUTA
Wakati wabunge wa Chadema wakikamatwa, wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), wamesema wanaunga mkono Ukuta, kwa sababu imelenga kupambana na uvunjaji wa demokrasia unaodaiwa kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. 

Msimamo huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Wabunge wa CUF, Riziki Mngwali alipozungumza na wanahabari kufuatia taarifa zilizosambaa kuwa wabunge hao wanapinga Ukuta. 

Riziki ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani, alisema wabunge wa chama hicho hawana tatizo na Ukuta na wanaunga mkono, hivyo tofauti na propaganda zinazoenezwa kuwa wanaupinga. 

“Chadema ni washirika wetu kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hivyo hatuna sababu ya kutowaunga mkono. 

 “Tunachosubiria ni taratibu za uongozi wa juu kukamilika kisha watupe mwongozo nini cha kufanya kwenye Ukuta. Lakini wabunge tupo pamoja na operesheni hii, hatuipingi kwa sababu ina lengo ya kudai haki na demokrasia inayominywa,” alisema Riziki.