Waziri Mkuu: Tanzania Iko Tayari Kujifunza Kutoka Nchi Nyingine.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania iko tayari kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo ni wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM) ili iweze kuboresha hatua ilizofikia kwenye mpango huo.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Agosti 26, 2016) wakati akichangia mada katika Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya InterContinental jijini Nairobi, Kenya.
“Nitumie fursa hii kukiarifu kikao chako kwamba Tanzania imeshaanza kutekeleza mpango kazi wa Kitaifa ambao umejikita kutatua changamoto katika sekta za maji, elimu, kilimo, nishati na miundombinu kama zilivyoainishwa kwenye kikao cha APRM,” alisema.
“Ili kuhakikisha kuwa zinafanyiwa kazi haraka, changamoto hizi za kisekta zimepewa kipaumbele kwenye Mpango wetu wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2016-2021 ambao umejikita zaidi kwenye viwanda,” aliongeza.
Tanzania ilifanyiwa tathmini yake Januari, 2013 kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Mapema, akifungua mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema viongozi wa Afrika hawana budi kukubaliana na kuungana kutafuta suluhisho katika ushindani wa kibiashara.
Alisema nchi wanachama wa mpango huo hawana budi kujenga umoja kama njia ya muafaka ya kufikia makubaliano hayo.
Wakati huohuo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema bara la Afrika linakabiliwa na changamoto 11 (strategic bottlenecks) ambazo zinakwamisha maendeleo ya bara hilo na akataka zitafutiwe ufumbuzi ili kuzisaidia nchi nyingi barani humo.
Akiwasilisha mada binafsi katika mkutano huo, Rais Museveni alisema kwa zaidi ya miaka 50, amekuwa kiongozi katika sehemu kadhaa na kwamba amebaini kuwa changamoto hizo zimezuia ukuaji wa uchumi barani Afrika pamoja na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Alisema asilimia kubwa ya changamoto hizo haikupata ufumbuzi hata wakati malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs) yalipokuwa yanatekelezwa.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni mikanganyiko ya kiitikadi ambayo huzaa ubinafsi na maslahi binafsi; kuwepo kwa mataifa dhaifu (weak states); nguvukazi duni (kitaaluma na kiafya), uduni wa miundombinu (barabara, maji, umeme, tehama) ambao unashindwa kuvutia uwekezaji; uhaba wa viwanda unaolazimisha nchi kusafirisha mali ghafi na uhaba wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa barani Afrika.
Changamoto nyingine ni uduni wa huduma za kijamii unaosababisha huduma mbovu kwenye maeneo ya utalii, mabenki na mahoteli; kilimo duni kisichotumia mbolea, dawa za kuua wadudu, mbegu za kisasa au njia za umwagiliaji; makosa ya kisera kama vile ubinafishaji au utaifishaji mali zinazomilikiwa na sekta binafsi; ukandamijazi wa demokrasia na ukosefu wa maadili miongoni mwa watumishi wa umma.
Naye Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema kwa vile changamoto hizo zinagusa nchi nyingi za Afrika, ni vema iundwe timu ya wataalamu watakazipitia zote na kuainisha zipi zinafaa kufanyiwa kazi na kisha taarifa yao iwasilishwe kwenye kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi wanachama.
Akifunga mkutano huo, Rais Kenyatta aliitaka sekretarieti ya APRM ipitie changaoto hizo na kuziwakilisha kwenye kikao chao kijacho ambacho alisema kitafanyika Januari 2017, mjini Addis Ababa, Ethiopia katika tarehe itakayopangwa baadaye.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, AGOSTI 27, 2016.
No comments:
Post a Comment