Waziri Mkuu: Wekeni majina ya mitaa Dodoma Mjini, Chamwino

MATANGAZO

MATANGAZO
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza mamlaka za serikali za mitaa nchini kuweka haraka majina katika barabara na mitaa katika maeneo yao, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi.

Waziri Mkuu pia ameelekeza taasisi za serikali kuzipa kipaumbele kwa Manispaa ya Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino katika Mkoa wa Dodoma wakati wa kutekeleza mpango huo.

“Dodoma na Chamwino ndio yawe maeneo ya kipaumbele wakati wa kutelekeza mradi hiyo kwani serikali imeshabainisha nia yake ya kuhamisha mji mkuu wa nchi kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma,” amesisitiza.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa maelekezo hayo jana wakati wa Uzinduzi wa Muongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa pamoja.

Amewataka mawaziri na mamlaka husika kukamilisha kuweka majina ya mitaa na barabara ifikapo Desemba, mwaka huu. Amezitaka taasisi za umma na binafsi, kuweka kipengele cha anwani za makazi ili kutekeleza mpango huo wa maendeleo.

Alizitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Wakala wa Barabara wa Tanzania (Tanroads), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) na Mipango Miji na Mradi wa Kuboresha Miji. Alisema mpango huo mpya utaboresha mpangilio wa miji, utasaidia masuala ya ulinzi na usalama, huduma za kijamii na kuboresha mazingira ya biashara na uchumi nchini.

“Itakuwa rahisi kukusanya kodi za serikali kwa sababu itakuwa rahisi kutambua na kufuatilia walipa kodi katika maeneo yao," amesema.

Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Posta ya Mwaka 2003 na Azimio la Umoja wa Posta Duniani (UPU) lililofikiwa Doha, Qatar mwaka 2012, lililotaka nchi zote duniani kuhakikisha kuwa kila mtu anakuwa na anuani. Kamu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Christine Mndeme alimhakikishia Waziri Mkuu kuwa mamlaka za Dodoma, zimeanza kutekeleza mpango huo wa kuweka anuani katika mitaani na kwenye barabara za mji huo mkuu.

“Mpango wetu Dodoma ni kuipa mitaa na barabara majina ya viongozi waliohai na waliokwishafariki kutokana na mchango wao hapa nchini kama vile Pius Msekwa, Job Lusinde, Hayati Rashid Kawawa na George Kahama,” alisema Mndeme.

Nchini Tanzania mradi wa majaribio, ulianzia Mkoa wa Dar es Salaam na Arusha na baadaye ulifuatia Mkoa wa Dodoma na mpango ni kukamilika Juni, 2018.