Kauli ya Mbowe yaikera Serikali......Waziri Amtaka Aache Kuingilia Madaraka ya Rais
Serikali imemjia juu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kutokana na kauli yake kuwa Rais John Magufuli amekuwa akipendelea baadhi ya kanda katika uteuzi wake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenister Mhagama jana Jumatatu jioni alisema Mbowe anapotosha na kumtaka aache kuingilia madaraka ya Rais.
Wakati akichangia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2018/2019, Ijumaa iliyopita Mbowe alienda mbali na kudai anaweza kuleta uthibitisho kama Bunge litamkata kufanya hivyo.
“Mumwambie bwana mkubwa unapoamua mambo mengine tenda haki pande zote. Lakini unapokuwa haki hiyo unaipeleka mahali fulani na unakandamiza upande mmoja unawanyima haki”
Mbowe alitolea mfano wa teuzi mbalimbali alizozifanya Rais Magufuli tangu aingie madarakani mwaka 2015, akisema hazikugawanywa kwa usawa wa mikoa kama utamaduni uliokuwepo awamu zilizopita.
Hata hivyo, jana Jumatatu jioni Jenister amesema Ibara ya 36 (1) (2)(3)(4) imempa Rais madaraka ya kuanzisha na kufuta ya nafasi za mbalimbali kwa utumishi na haijasema atazingatiwa usawa wa kanda.
“Ibara hiyo haisemi kuwa Rais wakati atakapokuwa anafanya uteuzi eti aangalie ukanda. Haisemi hivyo Ibara hiyo haisemi anavyoandaa uteuzi aaangalie makabila mbalimbali,”alisema Mhagama.
“Unasimamaje ndani ya Bunge kuhoji madaraka ambayo Rais amepewa kwa mujibu wa Katiba? Alihoji Mhagama na kutoa mifano ya teuzi tatu zilizofanywa na Rais kutoka mikoa ya Kaskazini.
“Ameteuliwa Aggrey Mwandry kutoka Siha kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na anafanya kazi vizuri sana. Ameteuliwa Alexander Mnyeti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara,”alisema na kuongeza
“Ameteuliwa Anna Kilango kutoka Same. Nina orodha ndefu lakini uteuzi huo unafuata madaraka ya kikatiba. Niwaombe sana wabunge tusiingile madaraka ya Rais aliyopewa kwa mujibu wa Katiba.”
Alisema Rais amekuwa akifanya teuzi mbalimbali kwa utashi wa hali ya juu na anateua watu wa kubeba dhamana ya kumsaidia kuongoza kwa niaba yake pasipo upendeleo.
No comments:
Post a Comment