Marekani yalalamika baada ya China kulipiza kisasi
Marekani imeutaja ushuru wa forodha uliowekwa na China kwenye bidhaa zake kama “sio haki”, baada ya China kuweka ushuru wa bidhaa 128 zenye thamani ya dola bilioni 3, zinazoingizwa na Marekani nchini humo.
Bidhaa, zilizowekewa ushuru na China, ni pamoja na matunda na nyama ya nguruwe, ikiwa ni hatua za karibuni zaidi za ulipizaji kisasi kufuatia Marekani kupandisha ushuru wa bidhaa za chuma cha pua na bati kutoka China.
Aidha, hatua hiyo ya China imekuja baada ya mvutano mkali kati ya nchi hizo kutokana na masuala ya kibiashara, ambapo hofu kubwa ilikuwa ni kutokea kwa vita ya kibiashara kati ya mataifa hayo yenye nguvu za kiuchumi duniani.
Serikali ya Rais Donald Trump imesema ushuru wake ulilenga bidhaa za chuma cha pua na bati zinazoingizwa nchini Marekani ambazo ilizichukulia kama tishio dhidi ya usalama wa taifa hilo.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Taro Kano akiwa mjini Tokyo ameelezea wasiwasi wake kwa kuhusiana na hatua hizo za kisasi kati ya Marekani na China, na kusema kwamba zinaweza kuwa na matokeo makubwa kiuchumi.
No comments:
Post a Comment