Mwigulu Aliagiza Jeshi la Polisi Kuwaweka Ndani Madereva Wanaosababisha Ajali
Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Mwigulu Nchemba amelitaka Jeshi la Polisi kuwaweka ndani madereva wanaosababisha ajali kutokana na mwendo kasi na baadaye kupelekwa Mahakamani.
Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo jana Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu muongozo wa Mbunge wa Ulanga Morogoro Mhe. Goodluck Mlinga, juu ya chanzo cha ajali ya basi la City Boy kutoka Karagwe Mkoani Bukoba kuelekea Dar es Salaam ambalo liligongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso lililokuwa linatoka Singida kuelekea Igunga usiku wa Aprili 04 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 12.
“Hatuwezi kuacha watu wanapotea kwa ajili ya uzembe wa mtu mmoja na kuleta hasara na vilio vikubwa kwa Watanzania,” alisema Dkt. Mwigulu.
Amesema, ajali nyingi zinazotokea hapa nchini zinasabishwa na mwendokasi na sio tatizo la miundombinu ambapo katika ajali zilizoripotiwa ajali 1500 zilisababishwa na mwendo kasi na ajali 89 zimetokana na miundombinu.
Aidha Dkt. Mwigulu amesema, Tanzania ni moja ya nchi zenye barabara bora hivyo ajali nyingi zinazotokea husababishwa na uzembe wa madereva pamoja na mwendokasi.
Wakati huohuo bungeni hapo, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali imeweka utaratibu mashuleni wa kuwawezesha watoto wa kike kuripoti matukio ya udhalilishaji na pia imeanzisha klabu mbalimbali za kuwajenge uwezo na ujasiri wa kuweza kuripoti matukio ya udhalilishaji.
Hata hivyo Prof. Ndalichako amewataka watoto kutokuwa na uwoga wowote kwa sababu Serikali yao inawalinda, hivyo pale wanapofanyiwa vitendo kinyume na matakwa ya Serikali watoe taarifa ili Serikali ichukue hatua stahiki kwa wale wote wanao wadhalilisha na kusababisha watoto wasisome kwa amani.
No comments:
Post a Comment