Pareso ‘akinukisha’ Bungeni
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cesilia Pareso amesema ukiacha maadui watatu wa Taifa ambao ni maradhi, umasikini na ujinga ameongezeka adui namba nne ambaye ni vyama vya siasa vya upinzani.
Akizungumza jana Alhamisi Aprili 5, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2018/19 bungeni mjini Dodoma, Pareso alisema vyama vya upinzani ni adui mwingine kwa kuwa kwa sasa vinapigwa vita na Serikali iliyopo madarakani, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kufanya shughuli za siasa.
Mbunge huyo pia amegusia chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni, kubainisha kuwa zilikuwa ni kati ya Chadema na Jeshi la Polisi sambamba na kueleza jinsi wabunge na madiwani walivyonunuliwa na kuvihama vyama vyao, nchi kulazimika kufanyika chaguzi nyingine alizodai aimegharimu zaidi ya Sh6 bilioni.
Maelezo ya Pareso yalipingwa na baadhi ya wabunge na wengine kumuunga mkono huku Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akimjibu mbunge huyo kuwahusisha polisi na chaguzi mbalimbali.
“Utaendeleaje kupima chama cha siasa kinakua kama hakifanyi mikutano ya hadhara na kuongeza wanachama, leo mtu anajiunga kesho mtu anatoka,” alisema Pareso.
“Kama mnakataza vyama vya siasa visifanye mikutano ya hadhara, hamuwezi kuja bungeni na kutueleza vyama hivi vimeendelea kufanya vizuri miaka 26 iliyopita.”
Huku akizungumza kwa upole Pareso alisema, “Miaka ya nyuma waasisi wa nchi hii waliwaaminisha Watanzania kwamba kuna maadui watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi lakini kwa yanayoendelea leo, jambo jingine limeongezeka kwa Serikali iliyopo madarakani. Adui mwingine ni vyama vya siasa.”
Alisema siku za hivi karibuni wabunge na madiwani wa vyama vya siasa, hasa upinzani wamekuwa wakiripoti polisi na kuwekwa rumande, hata kama wataachiwa wataendelea kuripoti polisi.
“Mmeongeza adui mwingine ambaye ni vayama vya siasa vya upinzani. Tumeshuhudia kwenye changuzi ndogo za marudi, utumiaji mbovu wa fedha za wananchi. Kama tulitenga fedha za dharura Sh4bilioni endapo utatokea uchaguzi leo tumetumia Sh6.9bilioni,” alisema.
“Kwanini tusingefikiria kuhifadhi hizi hela kuliko kurudisha wananchi kufanya chaguzi tena kwa sababu tu watu wameamua kununua watu warudi upande wa pili.”
Alisema chaguzi hizo za marudio zilikumbwa na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi, “tumeshuhudia uchaguzi kati ya Chadema na Jeshi la Polisi. Nilishuhudia wakala anatekwa kituoni polisi yupo na hasemi kitu.”
“Ushauri wangu kwa Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) kwa sababu inaonekana mmeongeza adui mwingine ambaye hamtaki kumsikia, ushauri wangu ni kuleta marekebisho ya katiba hapa bungeni. Tufute vyama vingi ili ulimwengu na dunia ijue kwamba Serikali haitaki vyama vingi turudi kwenye mfumo wa chama kimoja. Hiyo ni njia sahihi na mtaendelea kuyafanya mnayoyafanya kama mnavyotaka.”
Wakati Pareso akiendelea kuchangia, Mwigulu alisimama na kutoa ufafanuzi wa alichokisema mbunge huyo.
“Pamoja na kuheshimu uhuru wa kuongea na kulinda uhuru wa mbunge kutoa maoni yake, nilitaka kuwashauri wabunge tunapoongelea taasisi ambazo zipo kikatiba na kufanya kazi kwa ajili ya wananchi tuheshimu kazi zinazofanywa,” alisema Mwigulu.
“Hakuna uchaguzi kwa uzoefu wangu ambao utafanyika bila usalama kuimarishwa. Uhalifu wowote unaofanyika ndani ya nchi, iwe wakati wa uchaguzi au wakati ambao si wa uchaguzi, unahitaji kuwahakikishia wananchi usalama kama kawaida.”
Mwigulu alisema uzoefu umeonesha kuwa muongeaji (Pareso) chama chake kinaposhiriki katika uchaguzi kunakuwa na matukio makubwa ya uhalifu.
“Kuna uchaguzi mmoja chama chako (Chadema) hakikushiriki hakukuwapo na matukio ya aina yoyote ya utekaji wala maumivu ya wananchi. Sisi kama Jeshi la Polisi tupo kwa ajili ya kuwahakikishia wananchi usalama na hatuwezi kuacha wananchi wakakatana mapanga,” alisema.
Baada ya maelezo hayo Pareso aliendelea kuchangia, “Naomba kumwambia Mwigulu kwa sababu unaingia katika baraza la mawaziri, pokea ushauri wangu na umueleze Rais Magufuli tufute vyama vya upinzani nchini.”
No comments:
Post a Comment