Waziri Mwakyembe Awaasa Watanzania Kupambana Na Viashiria Vinavyo Sababisha Mauaji Ya Kimbari
Date: 8:59:00 AMNa: Mwandishi wetu
Waziri  wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe, amewaasa  Watanzania kuhakikisha wanapambana na viashiria vyote vinavyoweza  kusababisha uvunjifu wa amani na mauaji ya kimbari. Kauli hiyo  Dkt.  Mwakyembe ameitoa wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu za mauaji ya  kimbari yaliyotokea nchini Rwanda miaka 24 iliyopita.
Kwenye  hotuba yake Dkt. Mwakyembe amesema mauaji ya kimbari hayatokei ghafla  bali huanza kwa chokochoko na kauli za kichochezi ambazo zina lengo la  kuigawa jamii vipande vipande. 
“Kilichotokea  Rwanda ni fundisho kwetu, mauaji ya kimbari hayatakiwi kutokea tena.  Kuhakikisha hayatokei lazima tuyadhibiti mambo yote yanayoweza kuligawa  taifa kwa faida ya kizazi cha leo, kesho na keshokutwa” Dkt. Mwakyembe  alisisitiza.
Kuendelea  kutia mkazo wa ujumbe wake Dkt. Mwakyembe aliinukuu kauli ya Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, aliyoitoa  wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Rwanda  ambapo alisema “haya  hayatatokea tena, hatuwezi kubadili kilichotokea awali, lakini tunaweza  kubadilisha hali ya leo na hata ya baadae”.
Balozi  wa Rwanda nchini mheshimiwa Eugine Kayihura ameishukuru Serikali na  wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kuwa pamoja na Wanyarwanda. Pia  ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kindugu kati ya Tanzania na Rwanda  kwa maendeleo ya watu wake.
Kwa  upande wake Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez amesema  nchi zote zina wajibu wa kuwalinda wananchi wake dhidi ya mauaji ya  kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Pia zinatakiwa  kuhakikisha zinaungana kupambana na mtu au kikundi chochote chenye nia  ya kutekeleza uhalifu kama huo.
Kumbukumbu  za mauaji ya kimbari ya Rwanda huadhimishwa kila mwaka na mwaka huu  maadhimisho hayo kwa Tanzania yamefanyika ukumbi wa mikutano wa Mlimani  City ambapo Dkt. Mwakyembe alikuwa mgeni rasmi. Maadhimisho hayo  yalihudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali wakiwemo mabalozi  wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, watu mashuhuri, viongozi wa  serikali na mashirika ya kimataifa na wanafunzi wa shule za sekondari za  jijini Dar-es-salaam











































