CHADEMA Wapinga Kauli ya Jeshi la Polisi Kuzuia Mikutano ya Ndani ya Vyama vya Siasa

MATANGAZO

MATANGAZO
Wakati Jeshi la Polisi likisisitiza kupiga marufuku mikutano na maandamano ya Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta nchini (Ukuta), chama hicho kimepinga katazo hilo nakudai kuwa ni haramu kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo na Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Makao Makuu ya chama hicho Mtaa wa Ufipa, jijini Dar es Salaam.

Kwenye mkutano huo akiwa na Lawrance Masha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani (2005-2010) Lissu amesema, rais anayo nafasi ya kuzuia mikutano ya hadhara kwa sharti la kupeleka hoja bungeni na kisha kujadiliwa na si vinginevyo.

“Ipo sheria ya kutangaza hali ya dharura, iliyotungwa mwaka 1995, hii inamruhusu rais kupeleka hoja bungeni ya kutaka kutangaza hali ya dharura kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu na kama Bunge likiridhia, basi rais anatangaza, namshauri Magufuli afanye hivyo.

“Aitangazie Tanzania na dunia kwa ujumla kuwa, nchi hii ipo katika hali ya hatari na katika hali ya dharura, na kwamba mikutano yote itakuwa marufuku.

“Na miezi mitatu ikiisha aende tena bungeni kuomba aongeze mingine. Akifanya hivyo atakuwa hajavunja sheria na hata sisi tutamtii,” amesema Lissu.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kutoa matamko yanayoiingiza nchi katika utawala wa kidikteta.

Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku moja tu, tangu jeshi hilo kupitia Nsato Marijani, Kamishina wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, litangaze kupiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa nchini, ikiwemo vikao vya ndani vya vyama.

Katika mkutano na wanahabari, makao makuu ya chama hicho, akiwa ameambatana na Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Mjumbe wa Kamati Kuu, pamoja na Masha amesema, Lissu amesema, kamwe Chadema hakiwezi kuruhusu ukiukwaji wa katiba na sheria za nchi.

“Amri ya jana ya polisi, wakipiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa ikiwemo vikao vya ndani ni muendelezo wa amri haramu na kitendo hicho cha jana na vingine vilivyopita, ni mfano hai ya kwamba, nchi yetu imeingia katika mfumo wa udikteta.

"Kwani, kwa mujibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1967; udikteta ni utawala wa mtu mmoja au kikundi cha watu wachache wanaofikiria kwamba, amri zao ndiyo sheria na wote wanaowapinga, hukiona cha mtema kuni,” amesema Lissu.

Lissu amesema kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya sasa pamoja na sheria zote ikiwemo Sheria Na. 5 ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa, Sheria ya Maadili ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2007 pia sheria za Jeshi la Polisi, hakuna mahali ambapo polisi au rais anaruhusiwa kupiga marufuku mikutano ya kisiasa.

“Anayetakiwa kujulishwa kuhusu uwepo wa maandamano na mikutano ya hadhara ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) na kama kuna tatizo kwa muda huo, anaweza kuelekeza isifanyike kwa muda fulani lakini siyo Rais Magufuli wala Nsato,” amesema.

Wakati Lissu akisema hayo, Masha amesema, “nimekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa miaka mitano, lakini sikuwahi kupiga marufuku mikutano ya hadhara wala ile ya ndani. Nilifahamu kuwa, kuna umuhimu wa watu kuzungumza, kukosoana na kuelimishana.

"Ni vyema Rais Magufuli akajua, hii ni nchi ya kidemokrasia na kuna Katiba na sheria ambazo kila mtu ni lazima afuate akiwemo yeye, matamko ya kibabe ya Rais, Waziri wa Mambo ya Ndani na Jeshi la polisi ni kinyume na sheria pamoja na Katiba yetu.”

Dk. Mashinji, amesisitiza kuwa, Chadema kipo tayari kwa mazungumzo na mamlaka yoyote ya serikali juu ya azma ya kufanya mikutano na maandamano, ili mradi tu sheria na katiba ya nchi izingatiwe katika mazungumzo hayo.

“Hatujafunga milango ya mazungumzo na serikali, tunachosisitiza sisi ni kuwa hata kama kuna mazungumzo yatafanyika, Katiba na sheria za nchi yetu lazima zizingatiwe,” amesema Dk. Mashinji.