Tabia Tatu Kubwa Zinazoleta Tofauti Kati Ya Tajiri Na Maskini
Pia hata wanyama wengine wanapozaliwa iwe swala au simba wote huzaliwa wote wakiwa na nguvu sawa lakini utofauti huanza kujitokeza kwa jinsi wanavyoendelea kukua. Wengine hujikuta wana nguvu zaidi kuliko wengine na wengine hubaki wanyonge wanyonge.
Halikadhalika linapokuja suala la mafanikio mambo pia huwa yapo hivyo hivyo. Hii ikiwa na maana kwamba, kila binadamu amezaliwa sawa na binadamu mwingine. Hakuna binadamu ambaye atasema alikuja duniani akiwa na mafanikio na mwingine akiwa hana. Wote tulizaliwa tukiwa hatuna kitu.
Kama mambo yako hivi, ni nini kinacholeta tofauti hizi kubwa? Kwa nini wengine wawe matajiri na wengine wawe maskini? Je, matajiri wanakipi cha ziada kinachowafanya wafanikiwe? Kimsingi, huwa yapo mambo mengi kidogo yanayosababisha wengine wawe matajiri na wengine kuwa maskini.
Lakini katika makala haya tutaongelea mambo matatu ambayo yanahusiana na tabia ambazo zinaleta utofauti kati ya maskini na tajiri. Ni kweli zipo tabia ambazo matajiri wanazo na huwafanya wao kuwa matajiri kila kukicha. Ni tabia ambazo huwatenga kabisa na maskini na kuwaacha matajiri waendelee kufanikiwa.
Ikiwa utaamua kujifunza na kuzifatilia tabia hizi kwa karibu, uwe na uhakika utajiri utakuwa mikononi mwako muda sio mrefu. Nasema hivyo nikiwa na maana hii, ukitaka kuwa tajiri fanya yale ambayo matajiri wanafanya nawe utafanikiwa na kuwa kama wao.
Hebu kwa pamoja bila kupoteza muda, tuangazie nukta kadhaa, zinazoweza kutuonyesha tabia zinazowatenga kati ya matajiri na maskini.
1. Kuwekeza.
Watu wenye sifa ya utajiri ndani mwao hata kama bado hawajafika huko kwenye utajiri halisi ni wawekezaji wazuri sana. Si watu wa kuridhika na chanzo kimoja cha mapato. Wana vitega uchumi vingi sana ambavyo vinawasaidia kuingiza mapato kwa wingi hata kama wamelala.
Kwa mfano uatakuta wamewekeza kwenye mashamba, mafuta, migodi na maeneo mengine mengi. Hii ni sifa mojawapo kubwa inawatenga maskini na matajiri. Ukiona una kitega uchumi kimoja ujue unajizibia nafasi mwenyewe ya kuelekea kwenye utajiri mkubwa.
2. Kuweka akiba.
Suala la kuweka akiba kwa watu matajiri sio suala la hiari, kwao ni lazima. Angalau huweka asilimia kumi ya kile wanachokipata. Wanajua vizuri akiba hizo ni msaada mkubwa kwa baadae katika suala zima la kuwekeza. Wao katika kuweka akiba ni lazima, na pia hawana mchezo katika hilo.
Kutona na tabia hii, huwafanya wazidi kufanikiwa kila siku na kuwaacha maskini wakibaki kuwa maskini. Ni kitu ambacho unatakiwa kujifunza na kuelewa kwamba, akiba ni jambo la msingi sana kujiwekea kama unataka kuwa tajiri. Vinginevyo acha kuweka akiba, uendelee kubaki kwenye umaskini.
3. Kutoa.
Tabia nyingine inayowatenga watu matajiri na maskini ni ile hali ya kutoa. Watu matajiri ni watoaji wazuri sana wa pesa na mali zao. Hufanya hivi si kwa sababu wanazo nyingi, bali kutoa ni moja ya kanuni kubwa ya mafanikio walioamua kuitumia. Huwezi kufanikiwa sana kama hutoi.
Ieleweke hivi, maskini wanaendelea kubaki kuwa maskini kwa sababu ya uchoyo walionao. Hukumbatia sana walivyonavyo na kusahau kutoa. Kosa hilo huwafanya wazidi kuendelea kuwa maskini siku zote za maisha yao. Ili kuwa tajiri ni lazima kutoa.
Kumbuka, tabia ya kuwekeza, kuweka akiba na kutoa ni moja ya tabia kubwa zinazo watenga matajiri na maskini. Matajiri wanajikuta wakiwa ni watu wakuzifanyia kazi tabia hizo na kuwafanya kuwa matajiri na maskini hubaki na umaskini wao kwa sababu ya kutokuzifanyia kazi tabia hizo. Chukua hatua ya kutenda ili kubadili maisha yako.
No comments:
Post a Comment