Umoja wa Wanawake Wapinga Maandamano UKUTA Ya Chadema

MATANGAZO

MATANGAZO
Umoja wa Wanawake Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania (UWASATA), umepinga maandamano yasiyo na ukomo yaliyotanganzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa hayana tija kwa wananchi na Tifa kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa umoja huo Cecilia Augustino, alisema maandamano hayo yanaashiria uvunjifu wa amani ambayo ni urithi wa Taifa la Tanzania.

Alisema wamefikisha tamko lao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi na kumtaka msajili kutoacha chokochocko hizo ziendelee kwani zitasababisha kutoweka kwa amani nchini.

“Sisi wanawake viongozi wa vyama vya Siasa Tanzania tunapinga azimio la maandamano yasiyo na kikomo yanayoandaliwa na chama cha Chadema, hakika maandamano hayo hayana tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla” alisema Hokororo na kuongeza:

“Mheshimiwa Msajili, chokochocko hizi zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa zikiachwa tu bila ya kukemewa tunaamini tunu yetu ya amani ambayo ni urithi wetu tulioachiwa na waasisi wetu itatoweka”

Aliongeza kuwa hatma ya maandamano hayo ni kuingia kwenye machafuko na hatimaye mauaji na mateso kwa wanawake, watoto na walemavu, mambo ambayo hawatakubali yatokee.

Alibainisha kuwa wanawake viongozi wa vyama vya siasa wanaamini kuwa siasa ni kushindana kwa hoja na si uvunjifu wa sheria kwa njia ya maandamano yasiyo na tija kwa wananchi na Taifa.

Aliliomba Baraza la Vyama vya Siasa kuhakikisha linawajibika katika kulinda demokrasia, amani na ustawi wa jamii nzima ya Watanzania.

Katika hatua nyingine, umoja huo unaojumuisha wanawake viongozi wa vyama 22 vya siasa nchini, umeomba kufanya kongamano la amani lenye lengo la kuhamasisha amani na utulivu nchini.

Hivyo, Hokororo aliwaomba viongozi wakuu wa nchi kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, wadau wa amani na mashirika binafsi kushirikiana na umoja huo kufanikisha kongamano hilo.

“Hakika tunaumia wanasiasa wanapokuwa chanzo cha migogoro na vurugu kwa Taifa letu.Hivyo tunamuomba Rais wetu tunajua ni msikivu  aweze kuona namna nzuri ya kutafuta suluhu ya mgogoro huu wa kisiasa” alisema Mwenyekiti Cecilia Hokororo.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, tayari ameitisha Baraza la Vyama vya Siasa Agost 30, mwaka huu ili kutoa fursa kwa pande vyama husika kukaa meza moja na kujadili tofauti zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa umoja huo Ziada Athumani alisema wanaunga mkono hatua hiyo kwani ndio njia muwafaka ya pande husika ili kufikia muwafaka kwa njia ya amani.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, wanawake viongozi wa vyama vya siasa waliwakilishwa na wenzao kutoka vyama vya Demokrasi Makini, ADA TADEA na Chama cha Umoja wa Demokrasi ya Vyama Vingi (UMD).