Wabunge CUF Waunga Mkono UKUTA

MATANGAZO

MATANGAZO
WABUNGE wa Chama Cha Wananchi (CUF), wametangaza kuunga mkono maandamano yaliyoitishwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chini ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta), anaaandika Shabani Matutu.

Riziki Shari Mngwali, Mwenyekiti wa wabunge wa CUF amewambia wanahabari leo kuwa, upotoshaji kwamba wabunge wa chama chake hawaungi mkono maandamano hayo yanayotarajiwa kufanyika Septemba Mosi unapaswa kupuuzwa.

“Upotoshaji ambao umekuwa ukihusisha wabunge na chama kwa ujumla kwamba, hatupo tayari kushiriki katika maandamano hayo ya kupinga udikteta au hatuyaungi mkono ni taarifa zisizo na ukweli,” amesema.
Mngwali ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, amesema zaidi kuwa;

“tamko lilitolewa na Chadema ambao ni washirika wetu katika Ukawa, hivyo sisi tunaunga mkono mapambano yao na mtindo watakaotumia.
CUF tutakuja na mtindo wetu pia baada ya kufanikiwa kuziba nafasi za uongozi wa juu.”
Alisema kwamba, iwapo Chadema watawaomba CUF kushiriki kwenye shughuli zingine za Ukuta zinazoendelea watakuwa tayari kushiriki.

Mbarara Maharagande, mmoja wa maofisa wa CUF Makao Makuu, aliyekuwa ameongozana na kiongozi huyo amesema;

“Ukawa tumekuwa tukishirikiana katika mambo mengi ya msingi, hili la Ukuta tunaliunga mkono ila haibadilishi ukweli kuwa yale ni maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema na si Ukawa.”

Amesema wanaopotosha kuwa CUF haiungi mkono Ukuta wanashindwa kuelewa kuwa, operesheni Ukuta ni maazimio ya Chadema ambayo pia yanaungwa mkono na vyama washirika wa Ukawa.