Waziri Mkuu amwakilisha Rais katika Mkutano NAIROBI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasili Nairobi, Kenya jana kuhudhuria kwa niaba ya rais Dk John Magufuli mkutano wa Mkuu wa Sita wa Wakuu wa Nchi wa TICAD (TICAD VI) utakaofanyika Agosti 27 -28, mwaka huu.
Mapema jana Waziri Mkuu alikutana na viongozi wakuu mbalimbali wa makampuni kutoka Japan ambao watahudhuria mkutano huo akiwemo Makamu wa Rais wa Chiyoda Corporation Tadashi Izawa ambapo pamoja na kuangalia fursa nyingine katika sekta ya gesi Tanzania, kampuni hiyo imekubali kutoa mafunzo ya kujenga uwezo wa wataalamu kwa sekta ya gesi hususan usindikaji wa gesi kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi.
Waziri Mkuu pamoja na kumshukuru Bw. Izawa kwa mpango wao wa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania, amemtaka kuangalia uwezekano wa kuwasaidia vijana wanaotoka maeneo husika yenye gesi ili wapatiwe mafunzo ambayo yatawawezesha kumudu baadhi ya kazi kwenye viwanda vya kusindika gesi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Japan (JICA), Hiroshi Kato na kujadiliana mambo kadhaa yakiwemo ya nishati na miundombinu.
No comments:
Post a Comment