Tanzania yaongoza duniani kwa utoaji wa huduma za kifedha kwa kutumia simu

MATANGAZO

MATANGAZO

Tanzania imetajwa kuwa nchi ya kwanza duniani kufanikiwa katika utoaji wa huduma za kifedha kwa kutumia mitandao ya simu.

Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) Eng. James Kilaba katika mkutano wa kimataifa wa wadau wa mawasiliano ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU) kwa kushirikiana na TCRA pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

“Huduma za kifedha kwa mfumo wa digitali nchini Tanzania imepiga hatua kubwa ,ni nchi ya kwanza tuseme ulimwenguni kwa kutuma fedha na kutoa kwa njia ya simu bila matatizo yoyote, pia kuna mfumo wa kutuma fedha benki kwa kutumia mitandao ya simu,” alisema.

Kuhusu mkutano huo wa kimataifa ulioshirikisha washiriki zaidi ya 150 kutoka nchi mbalimbali duniani ambazo ni wanachama wa ITU, alisema umelenga kujadili namna ya kufikisha huduma za kifedha kwa njia ya simu katika sehemu ambazo hazifikiwi na huduma hiyo.

“Mkutano huu unasimamiwa na shirika la mawasiliano duniani ITC ambao umelenga kujadili namna ya kutumia mitandao ya simu kupeleka huduma za kifedha katika maeneo yasiyofikiwa na huduma za kifedha hasa ambako hakuna mabenki. Mkutano huu nchi imeamua kuuanda kwa ushirikiano wa TCRA na BOT, ” alisema.

Naye Gavana Mkuu wa BOT Profesa Benno Ndulu alisema hadi mwisho wa mwezi Julai mwaka huu takribani watanzania milioni 21.5 nchi nzima wanatumia huduma za kifedha kwa njia ya mitandao ya simu.

“Hadi kufikia Julai, 2016 watanzania 21.5 milioni wanatumia mitandao ya simu walau mara 1 kwa mwezi idadi hii ni kubwa na kwamba inaonesha sekta hii inakua kwa kasi,” alisema.

Profesa Ndulu alisema kuwa huduma za kifedha kwa njia ya mitandao ya simu imesaidia kukuza uchumi wa nchi.

“Malipo ya fedha kwa njia ya simu yanasaidia kupunguza gharama hivyo na kuwa kichochea cha maendeleo, sasa hivi wafanyakazi, wakulima, wanaotumia huduma za bima, wanaonunua bidhaa hulipa kwa Kutumia simu za mkononi hususani kwamba muda ndio muhimu,” alisema.

Aliongeza kuwa “Mitandao ya simu haiathiri huduma za kibenki, na benki wamechangamkia kutumia mitandao kufikia wateja wao, hutumia mawakala kufungulia account, mitandao hii husaidia benki kufikia wateja kote nchini, woga huo umepungua kwa sasa,”