Wilaya 43 ziko Hatarini Kukumbwa na Njaa

MATANGAZO

MATANGAZO


Serikali imesema kuwa nchi ina hifadhi kubwa ya chakula kutokana na mavuno ya msimu uliopita ingawa kuna wilaya 43 zenye upungufu wa chakula kutokana na mavuno yao kuwa chini hali iliyosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha amesema hayo jana wakati akizindua tovuti ya wakala wa hifadhi ya chakula nchini (NFRA) mjini Dodoma.

Mhe. Ole Nasha amesema kuwa kwa sasa serikali ipo katika hatua za mwisho za kuratibu uuzaji wa chakula nje ya nchi bila kuathiri hifadhi ya chakula na kuwatoa hofu wananchi wenye wasiwasi wa kukumbwa na baa la njaa.

Naibu waziri huyo ameongeza kuwa kwa tathmini waliyoifanya imebaini kuwa nchi nyingi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula hivyo serikali itatengeneza mifumo mizuri ya kupeleka chakula hicho nje ya nchi.

Baada ya kuzindua tovuti hiyo ya wakala wa chakula nchini, uhifadhi wa nyaraka za serikali kwa njia ya makaratasi umepitwa na wakati lakini pia akaongeza kuwa hata wizara nyingine zimeanzisha tovuti lakini ni kama zimekufa kwa sababu haziweki taarifa za mara kwa mara.