Repoa yatoa tahadhari kuhusu uchumi wa nchi

MATANGAZO

MATANGAZO
Taasisi ya Utafiti Repoa imetoa tahadhari ikisema licha ya juhudi zinazoendelea katika mageuzi ya kiuchumi, Serikali inapaswa kushughulikia vikwazo vilivyopo ili kukabiliana na ushindani wa masoko nje ya nchi.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Dk Donald Mmari alisema jana kuwa, pamoja na Serikali kushughulikia ukuaji wa uchumi kwa miaka 15 iliyopita, tafiti mbalimbali zinaonyesha viwango vya tija katika sekta nyingi ziko chini.

“Lakini pia hata ushindani wake ukilinganisha na nchi nyingine bado hauridhishi, Tanzania inao uwezo wa kujiweka katika nafasi kubwa zaidi kiuchumi duniani kutokana na upatikanaji wake katika jiografia, wingi wa rasilimali za asili, utulivu wa kisiasa na kijamii,”alisema.

Baadhi ya vikwazo alivyotaja katika mkutano wa waandishi wa habari ni pamoja na upatikanaji wa nguvu kazi yenye afya, ujuzi na elimu, miundombinu rafiki ya biashara na uwekezaji.

Wachumi kutoka taasisi mbalimbali, NGO, viongozi, wasomi, wahisani na watunga sera wametajwa kushiriki warsha itakayofanyika leo na kesho itakayojikita katika uzalishaji wenye tija na ushindani katika utandawazi.

Warsha hiyo itaongozwa na katibu mtendaji wa Shirikisho la Forodha la Kusini mwa Afrika (Sacu), Pauline Mbala huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.).

Masuala yatakayojadiliwa yatajikita kwenye mabadiliko ya mfumo wa uchumi hususan katika umuhimu wa kufahamu misingi ya uzalishaji wenye tija na ushindani katika utandawazi na masoko

Mtafiti mwandamizi katika taasisi hiyo, Dk Blandina Mlama alisema ni umuhimu pia kuwekeza katika mnyororo wa thamani kupitia sekta zinazoajiri Watanzania wengi.