Wananchi Waiomba Serikali Iwatatulie Kero
Wakazi wa Kijiji cha Kasumo, wilayani Buhigwe, mkoani Kigoma, wameiomba serikali iwatatulie kero mbalimbali zinazokikabili kijiji chao ikiwemo huduma za afya, maji, Elimu na Barabara.
Wametoa kilio hicho kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, mara baada ya kuwasili katika kijiji hicho ambapo pamoja na mambo mengine amewasisitiza watanzania kulipa kodi na kudai risiti wanapofanya manunuzi ya huduma na bidhaa.
Kijiji cha Kasumo, ndiko alikozaliwa Waziri huyo wa Fedha na Mipango, ambapo pamoja na wakazi hao kumpa kiongozi huyo mapokezi Makubwa, wakapeleka kilio serikalini ili waboreshewe huduma mbalimbali za kijamii.
Akijibu hoja za wakazi wa Kijiji hicho, Dokta Philip Mpango amewahimiza kufanyakazi kwa bidii ili wajikwamue kutoka katika lindi la umasikini na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ikiwemo kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili kujiletea maendeleo.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk, Philip Mpango, yuko mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi akihimiza uadilifu wa watendaji wa serikali waliopewa dhamana ya kukusanya kodi, matumizi ya mashine za Kieletroniki za kukusanyia kodi na kuelezea miradi ya kipaumbele ya serikali ya awamu ya tano ya kuwaletea wananchi maendeleo.
No comments:
Post a Comment