Tunde Lissu Sasa Anaweza Kutembea Mwenyewe, Kuoga
Afya ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji, inazidi kuimarika na sasa anaweza kufanya mambo mengi mwenyewe ikiwamo kwenda kuoga na kutembea kwa kutumia magongo.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), alipelekwa Ubelgiji Januari 7, mwaka huu, akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu tangu Septemba 7, mwaka jana.
Mbunge huyo aliumia vibaya baada ya kushambuliwa kwa risasi 32 na watu wasiojulikana nyumbani kwake mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana, tano kati ya hizo zikimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili.
Vinceti Mghwai, ambaye ni mdogo wa Lissu, alisema jana kuwa Lissu ameanza kutembea mwenyewe kwa kutumia magongo na kujipatia huduma mbalimbali ikiwemo kwenda kuoga bila msaada wa mtu mwingine.
"Tunamshukuru Mungu sana, Lissu anaendelea vizuri... tangu ameanza kupatiwa matibabu na mazoezi ya viungo tunaona mabadiliko makubwa mno," alisema na kueleza zaidi:
"Maendeleo ni makubwa sana, kuna vitu alikuwa hawezi kuvifanya lakini sasa anaweza kuvifanya mwenyewe kama kuoga. Siku za nyuma alikuwa akipelekwa maliwatoni lakini sasa hivi anatembea na magongo mwenyewe kwa kukanyagia mguu chini.
"Anakula mwenyewe.Tunaamini atatengamaa mapema zaidi, (na) haya kwetu ni maendeleo makubwa."
Mghwai alisema Lissu anapata muda mwingi wa kupumzika na huenda hiyo ndiyo ikawa sababu kubwa ya yeye kuendelea kupona haraka kutokana na kupatiwa matibabu na bila usumbufu wowote.
Alisema Lissu anapata matibabu katika mazingira tulivu tofauti na alipokuwa Hospitali ya Nairobi ambako alikuwa akisumbuliwa na makundi ya watu waliokuwa wakienda kumjulia hali.
"Kwa sasa ana muda wa kutosha kufanyiwa matibabu ya mazoezi, madaktari wanamfanyia mazoezi muda wote kwa sababu hakuna watu wanaokwenda kumuona na ndiyo sababu anaendelea kupona haraka," alisema Mghwai.
"Ubelgiji muda wote yuko na madaktari akipatiwa matibabu hasa mazoezi ya viungo... huku ni kazi kazi tu. Na madaktari waliahidi kufanya kazi.
"Kule Nairobi wakati mwingine alikuwa akiwaambia madaktari wamuache pale anaposikia maumivu wakati wa mazoezi lakini sasa hakuna kitu kama hicho na wamemwambia avumilie apone."
Kuhusu risasi iliyobakia kwenye nyonga, Mghwai alisema madaktari wa Ubelgiji hawataitoa na wataiacha kwa sababu walishaeleza kuwa haiwezi kuwa na madhara kwake kiafya.
"Kule Ubelgiji kazi kubwa ni kumfanyisha mazoezi ili sasa aweze kurejea katika hali yake na ndicho ambacho wanaendelea nacho na kwa kweli tumeanza kuona maendeleo makubwa."
Kuhusu gharama za matibabu, Mghwai alisema, zaidi ya Sh. milioni 100 zinatumika kila mwezi kwa ajili ya kumtibu na kwamba hadi sasa Bunge halijatoa fedha na familia inafuatilia lakini wamekuwa wakizungushwa huku na kule.
Alisema fedha zinazotumika kwa ajili ya matibabu yake ni zile zilizochangwa na wadau mbalimbali na wamekuwa wakifanya harambee kadhaa za kuchangia.
"Gharama ni kubwa sana kwa mwezi analipia zaidi ya milioni 100 katika hospitali hiyo na kama atakaa miezi miwili tutatumia zaidi ya milioni 200 na hizi ni fedha za matibabu pekee," alisema Mghwai.
Alieleza zaidi kuwa fedha zilizochangwa hazitoshi kumtibu Lissu na kwamba kwa sasa wadau wamesitisha kutoa michango baada ya tetesi kuwa serikali inagharamia matibabu yake.
Alisema familia inaendelea na juhudi za kuchangisha fedha zaidi ili kukamilisha matibabu yake.
"Tunaamini hakuna kitakachoharibika kwa sababu tumeshaweza kumponya tunaamini atakuwa mzima."
Alisema gharama kamili za matibabu na fedha zilizopatikana kwa ajili ya matibabu ya Lissu zinaweza kuzungumzwa katika vikao vya makubaliano na si yeye peke yake kuzungumzia.
Lissu ambaye Januari 6 alizungumza na waandishi wa habari akiwa nje ya Hospitali ya Nairobi, ikiwa ni siku moja kabla ya kusafiri kuelekea nchini Ubelgiji, alieleza kuwa alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 20 na 16 zilimjeruhi maeneo mbalimbali ya miguu, mikononi na kwenye nyonga.
Lissu alisema kutokana na shambulio hilo alifanyiwa operesheni 17 zilizofanikisha kuondoa risasi saba zilizoingia mwilini huku risasi moja ikisalia.
Wataalam wa afya walimshauri kuiacha risasi hiyo iliyopo kwenye nyonga wakisema kuwa inaweza kuleta madhara zaidi kama watajaribu kuitoa.
No comments:
Post a Comment